Wagonjwa mahututi wa Covid-19 wana uwezekano mkubwa wa kufa barani Afrika kuliko eneo lingine lolote ulimwenguni.
Utafiti uliochapishwa na jarida la The Lancet unaashiria hali hii kutokana na uhaba wa vifaa muhimu katika hospitali ambazo zinasaidia kuokoa maisha na pia uhaba wa wafanyikazi waliobobea.
Karibu 48% ya wagonjwa waliolazwa hospitalini barani Afrika wanakufa, ripoti inabainisha, ikilinganishwa na wastani wa ulimwengu wa 31.5%.
Na kiwango kinaweza kuwa cha juu zaidi katika hospitali za kiwango cha chini ambazo hazina vitengo vya uangalizi wa karibu.
"Utafiti wetu ni wa kwanza kutoa picha kamili juu ya kile kinachotokea kwa watu ambao wanaumwa sana na Covid-19 barani Afrika, na data kutoka nchi na hospitali nyingi," Prof Bruce Biccard kutoka Hospitali ya Groote Schuur na Chuo Kikuu cha Cape Town alisema.
"Kwa kusikitisha, inaonyesha kuwa uwezo wetu wa kutoa huduma ya kutosha umeathiriwa na uhaba wa vitanda vya wagonjwa mahututi na rasilimali chache ndani ya vitengo vya wagonjwa mahututi," Prof Biccard, ambaye aliongoza utafiti huo, aliongeza.
Zaidi ya vifo 120,000 vya Covid-19 vimeripotiwa barani Afrika sawa na 4% ya vifo vilivyoripotiwa ulimwenguni.
Zaidi ya watu wazima 3,000 kutoka nchi 10 za Afrika walishiriki katika utafiti huo ambao ulilenga hospitali 64 katika nchi 10 - Misri, Ethiopia, Ghana, Kenya, Libya, Malawi, Msumbiji, Niger, Nigeria na Afrika Kusini.
Utafiti huo uligundua kuwa kati ya Mei na Desemba mwaka jana, nusu ya washiriki walifariki bila kupewa oksijeni na wengine 10% hawakupata matibabu ya figo.

No comments:
Post a Comment