Na Ahmad Mmow, Lindi.
Baada ya serikali kufanikiwa kwakiasi kikubwa kudhibiti ujangili na kusababisha tembo kuwa salama na kuzaliana kwa wingi. Sasa kilio kimegeukia kwa wakulima, ambapo sasa tembo wamekuwa tishio na kusababisha vilio kwa wakulima.
Miongoni mwa maeneo ambayo wanasababisha vilio kwa wakulima kutokanana kuharibu mazao ya kilimo ni kijiji cha Chingulungulu, kata ya Namatutwe, wilaya ya Masasi mkoa wa Mtwara.
Hayo yameelezwa kwa nyakati na maeneo tofauti katika kata ya Namatutwe. Wakati viongozi na wananchi walipozungumza na Muungwana Blog.
Mkulima Prisca Kajile ambaye ni mmoja wa waathirika wa tembo hao alitoa wito kwa serikali iwalipe fidia waachie maeneo hayo ili fedha watakazolipwa watumie kununue maeneo mengine.
Alisema kila mwaka wanapata hasara na wanakuwa nawakati mgumu kimaisha.
'' Mwaka jana mazao yetu yaliliwa na tembo, mwaka huu vilevile. Lakini serikali haijawahi kutulipa fidia, kwamadai tumelima jirani na hifadhi. Sasa itulipe tuhame, maana walituambia tumwage pilipili na oili lakini hakuna chochote hata tangi la oili lenyewe lilipasuliwa na tembo,'' alisema Kajile.
Maelezo ya Kajile yaliungwa mkono na mwenyekiti wa kitongoji cha Mnalimbe, Saidi Lukanga ambae alisema takribani mashamba 30 yameharibiwa na wanakesha kuwafukuza.
'' Wakifukuzwa wanarudi, umbali baina ya kijiji cha Chingulungulu na hifadhi na yalipo mashamba haufiki mita miatano, tunaomba umbali wa mpaka uongezwe,'' alisema Lukanga.
Mwenyekiti wa serikali ya kijiji cha Chingulungulu, Kayusi Said Bakari ambaye pia aliomba upana wa mpaka baina ya kijiji hicho na hifadhi upanuliwe alisema tatizo la tembo halipo katika kitongoji cha Mkalimbe peke yake bali kijiji chote cha Chingulungulu.
Alisema licha ya jitihada za askari wa wanyama pori za kuwafukuza lakini tembo hao wamekuwa wakirudi na kuharibu mazao, ambapo tayari mashamba ya kaya takribani 67 yameharibiwa.
Kayusi alisema sababu ya tembo hao kurudi na kuharibu mashamba ni kutouwawa. Kwani wanafukuzwa tu.
Nae ofisa mtendaji wa kata ya Namatutwe, Gadaph Mtauni licha ya kukiri kuwepo changamoto hiyo katika kata yake alisema wamepeleka omba la kupanua umbali kutoka mpaka wa sasa hadi hifadhi ya Msanjesi. Nakwamba suala hilo limefikishwa hadi katika ngazi ya halmashauri ya wilaya ya Masasi kupitia baraza la madiwani la halmashauri hiyo.
Hatahivyo ofisa mtendaji huyo alisema miaka miwili iliyopita hali ilikuwa ni mbaya ikilinganishwa na msimu huu.
Kwaupande wake mhifadhi wa hifadhi ya Msanjesi, Mmunu Nduguru alikiri kwamba umbali kutoka yalipo mashamba hadi hifadhi haufiki hata mita mia moja. Hata hivyo suala la kupanua mikapaka ni suala la kisheria. Kwahiyo viongozi wafuate taratibu za kisheria ili ombi lao liweze kushughulikiwa kwamujibu wa sheria.
Aidha Nduguru alisema kuwauwa ni baada ya jitihada zote kushindikana. Bali kinachotokea katika maeneo hayo siyo kwamba tembo wanaofukuzwa wanarudi tena. Bali tembo hao wapo katika makundi tofauti.
Alitoa wito kwa wakulima kufanyia kazi elimu wanayopewa kuhusu namna ya kuwazuia tembo wasiingie mashambani. Huku akiweka wazi kwamba kumekuwa na mwitikio mdogo wa wananchi kuhudhuria mikutano ambayo inatumika kuwapa elimu.
'' Kumekuwa na mwitikio mdogo, wanahisi serikali inataka kuwanyang'anya mashamba yao,'' alisema Ndunguru ambae aliahidi kuendelea kutoa ushirikiano wa kuwadhibiti tembo hao.
Juhudi za kumpata mkuu wa wilaya ya Masasi ili kujua mpango wa serikali ya wilaya hiyo kuhusu tatizo hilo na ukubwa wa tatizo hilo katika wilaya yake zinaendelea.

No comments:
Post a Comment