Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo imeamuru kuwahamisha watu kutoka mji wa mashariki mwa taifa hilo Goma, baada ya volcano kulipuka katika mlima Nyiragongo uliopo karibu na mji huo wa mpakani.
Waziri wa habari Patrick Muyaya aliandika kwenye ukurasa wake wa Twitter kwamba operesheni ya kuwaokoa watu kutoka eneo hilo imeanza.
Lakini hata kabla ya tangazo hilo, maelfu ya wakaazi wa mji huo walikuwa wameanza kuondoka huku wakibeba vitu vichache walivyoweza kunusuru Gavana wa kijeshi wa jimbo la Kivu Kaskazini ambako Goma ni mji mkuu Jenerali Constant Ndima amethibitisha kuwa volcano hiyo ya Nyiragongo ilianza kuripuka saa moja jioni Jumamosi ikirusha lava yake.
Mara ya mwisho volcano hiyo iliripuka Januari mwaka 2002 na zaidi ya watu 100 waliuawa. Mripuko mbaya zaidi wa volcano hiyo ulitokea mwaka 1997 ambapo zaidi ya watu 600 waliuawa.

No comments:
Post a Comment