Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi, Dkt. Leonard Chamuriho, amewataka Wafanyakazi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), kuepuka majungu, fitina na makundi katika maeneo ya kazi na badala yake kufanya kazi kwa kushirikiana ili kuleta ufanisi na tija kwa Mamlaka hiyo naTaifa kwa ujumla.
Akizungumza katika Kikao cha 29 cha Baraza Kuu la Wafanyakazi wa Mamlaka hiyo, kilichofanyika mkoani Morogoro, Waziri huyo amewasisitiza Wafanyakazi hao kushirikiana katika kupinga vitendo vya wizi na rushwa kwa kufanya kazi kwa weledi na bidii pamoja na kulinda kwa nguvu zote mahusiano mema baina yao.
“Ni imani yangu kwamba katika kutekeleza majukumu yenu mliyopewa na Serikali, mtaendeleza utaratibu wa kushirikiana kati ya Menejimenti na chama chenu cha Wafanyakazi (DOWUTA), kulinda maslahi ya Taifa ndani ya Bandari, kwa kupinga vitendo vya rushwa na wizi”, amesema Chamuriho.
Ameongeza kuwa, kila mmoja anatakiwa kuheshimu nafasi ya kila mtu katika eneo la kazi kwani majukumu yao yanategemeana katika kufikia malengo ya Mamlaka hiyo.
Amewasisitiza wajumbe wa Baraza hilo kutumia kikao hicho, kupitia kwa makini mpango na bajeti yao, kushauri na hatimae kuja kusimamia utekelezaji wake.
Ameitaka Menejimenti na wawakilishi wa Chama cha wafanyakazi cha Mamlaka hiyo, kuwajibika kwa kuhakikisha kuwa wafanyakazi wote wa Mamlaka wanatambua na kutimiza wajibu wao ipasavyo pamoja na kusimamia maadili ya utumishi wa umma ili kuongeza ufanisi na tija.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka hiyo, Erick Hamisi, amesema tashirikiana na wafanyakazi wa TPA ili kufikia malengo ya Taasisi waliyojiwekea.
Kikao hicho cha 29 cha Baraza Kuu la Wafanyakazi wa TPA kina dhima kuu ya kujadili masuala ya bajeti, utendaji, uendeshaji wa bandari na utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayofanywa na Mamlaka hiyo.



No comments:
Post a Comment