Na Ezekiel Mtonyole - Dodoma.
Naibu Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia Mhe. Omary Kipanga amewataka watumishi waliopo katika Wizara hiyo kuzingatia nidhamu, ubunifu, maadili na weledi katika kazi zao ili kukuza kiwango cha elimu hapa nchini.
Naibu Waziri Kipanga ameyabainisha hayo jijini Dodoma wakati akifunga mkutano wa 28 wa Baraza la 10 la Wafanyakazi wa Wizara hiyo amewataka watumishi hao kuzingatia yale yote waliyoelekezwa na Waziri wa wizara hiyo, Prof Joyce Ndalichako jana wakati akifungua baraza hilo.
Ametoa rai kwa vyama vya wafanyakazi kama Tughe na Chama cha Walimu Tanzania CWT kushirikiana na Menejimenti ya Wizara kuhakikisha wanasimamia ipasavyo nidhamu na kukuza ubunifu kwa wafanyakazi lengo likiwa ni kuifanya wizara izidi kufanya vizuri kama ambavyo ilisifiwa na Rais Samia Suluhu Hassan.
" Nasisitiza mshikamano baina yetu watumishi, ili tuzidi kupongezwa kwa kufanya kazi vema ni lazima tushikamane tukiwa wamoja na wenye upendo, niombe kwa pamoja tuwe mabalozi wazuri wa kusimamia nidhamu na uwajibikaji kwenye vituo vyetu vya kazi.
Wizara yetu ndio uti wa mgongo wa Taifa letu, bila kukuza kiwango cha elimu na kuzalisha watalaamu wengi nchini ni vigumu kama Taifa kupata maendeleo, ni vema tukatoka na mkakati wa kuhakikisha tunazalisha vijana wasomi wenye tija kwa Taifa letu katika kuajiriwa na kujiajiri wenyewe," Amesema Kipanga.
Awali Katibu Mkuu wa Wizara hiyo ambaye pia ndiye Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi, Dk Leonard Akwilapo ameahidi kuwa watayafanyia kazi maelekezo yote yaliyotolewa kwao na Waziri viongozi wa ngazi za juu.
Nae Mwenyekiti wa Tughe, Archie Mntambo amesema wataendelea kufanya kazi kwa bidii na ufanisi mkubwa ili kulinda sifa ya wizara hiyo ambayo imekuepo kiasi cha kupokea sifa kutoka kwa Rais Samia.
" Nikuhakikishie Naibu Waziri yale yote mliyotuelekeza tutayafanyia kazi kuhakikisha tunakua wabunifu, wenye weledi na nidhamu katika kazi lengo likiwa ni kuzalisha kundi kubwa la vijana wasomi wenye tija kwa Taifa letu," Amesema Mntambo.

No comments:
Post a Comment