MBUNGE wa Jimbo la Mlimba mkoani Morogoro, Godwin Kunambi ameiomba serikali kuangalia upya mgawanyo wa miundombinu ya huduma ya afya na elimu kitaifa ambapo amesema kuna changamoto ya miundombinu kwenye sekta hizo.
Kunambi ameyasema hayo jijini Dodoma leo wakati akichangia hotuba ya bajeti ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tamisemi ambapo amesema kwa mfano Jimbo lake la Mlimba lina changamoto ya vituo vya afya kwani vipo viwili kwenye Halmashauri hiyo yenye kata 16.
Kunambi amesema kwa kuthamini sekta ya Afya kutokana na umuhimu wake yeye kama Mbunge kwa kushirikiana na wananchi wake wamekamilisha ujenzi wa Kituo cha Afya Kata ya Chita jengo la wagonjwa wa nje (OPD) na hivyo kumuomba Waziri wa Tamisemi, Ummy Mwalimu kuwasaidia kuwaletea Madaktari na wahudumu wa afya ili waweze kufungua kituo hiko.
" Wananchi wa Halmashauri ya Mlimba ni wachapakazi na wanapenda maendeleo, kauli mbiu yetu ni kwamba tunaanza wenyewe Serikali itatukuta, ujenzi wa jengo la wagonjwa wa nje katika Kituo cha Afya Chita umekamilika, tunaomba Mhe Waziri Ummy unapokuja kuhitimisha bajeti yako siyo mbaya ukisema unakwenda kuhitimisha kituo chetu ili wananchi wa Chita na maeneo mengine ya Jimbo la Mlimba waweze kupata huduma za afya.
Kwenye eneo hili la afya pia nikuombe Waziri Ummy tufanye tathimini wapo wanaopewa nafasi hizi kwenye ngazi za Halmashauri hawana sifa sasa tufanye tathmini Halmashauri kwa Halmashauri tuangalie leseni za waganga wa vituo vya afya tuone elimu yake, tufanye tathmini ya kitaifa," Amesema Kunambi.
Amesema Ikama ya watumishi wa sekta ya afya kwenye Halmashauri ya Mlimba mahitaji ni watumishi 432 lakini waliopo ni 169 pekee na hivyo kushindwa kuwahudumia wananchi ipasavyo kutokana na kuzidiwa na hivyo kumuomba Waziri Ummy kuliangalia hilo pia kwa umuhimu ili Ikama ya watumishi wa afya iendane na mahitaji ya wananchi.
Kuhusu Zahanati Mbunge Kunambi amesema tayari kwa kushirikiana na wananchi wake wameshajenga maboma takribani 10 kwenye kata mbalimbali za Halmashauri hiyo na hivyo kumuomba Waziri Ummy tena kuwaunga mkono wananchi hao kwa kumalizia ujenzi huo ili waweze kunufaika na serikali yao.
Katika sekta ya Elimu, Kunambi amesema kwenye elimu ya msingi tayari wameshajenga maboma ya madarasa 41 na hivyo kuiomba serikali iwaruhusu kama imepanga kuwaletea fedha za madarasa basi fedha hizo wazitumie kukamilisha kukamilisha maboma hayo kwanza.
" Kwenye sekta ya Elimu pia tuna changamoto ya Ikama, mahitaji yetu ni walimu 1,420 lakini waliopo ni 654 hivyo tuna upungufu wa walimu 766 sasa tungeomba maeneo haya yatiliwe mkazo kwani yanalenga mustakabali wa maisha ya watoto wa kitanzania ambao kesho yao ipo mikononi mwa elimu kwa maslahi yao wenyewe na Taifa letu kwa ujumla," Amesema Mbunge Kunambi.

No comments:
Post a Comment