Wanachama wa Chama cha Wafanyabiashara wenye Viwanda na Wakulima (TCCIA) mkoa wa Pwani wameshauri Katiba yao iandikwe kwa lugha ya Kiswahili badala ya Kiingereza kama ilivyo sasa ili kila mtu aweze kuelewa vizuri miongozo, kanuni na sheria zinazowaongoza .
Ushauri huo umetolewa leo Februari 28 mjini Kibaha wakati wa mkutano mkuu wa chama hicho wenye ajenda ya uchaguzi huku wanachama mbalimbali wakitoa mawazo yao ya kuendeleza umoja huo ili kufikia malengo yao ya kujikwamua kiuchumi.
Mkazi wa Mlandizi, Asha Saidi amesema katiba iliyopo ambayo imeandikwa kwa Kingereza inawata taabu ya kuelewa kilichoandikwa kwa sababu wanachama wengi wana elimu ya chini, jambo ambalo wamesema linapunguza ushiriki wao katika masuala mbalimbali ikiwemo kugombea nafasi za uongozi.
“Tumeshangaa msimamizi wa uchaguzi, Joseph Kahungwa kutangaza nafasi ya mtunza fedha ipo wazi hakuna aliyeoomba na nafasi nyingine yupo mtu mmoja mmoja tu wakati tunaamini kabisa wataalamu wapo na pengine ni watoto wetu lakini kwa kushindwa kutafsiri katiba tumekwama kujaza fomu ama hatujui majukumu, hivyo, tunaomba tuwe na katiba pia ya lugha ya Kiswahili,” amesema.
Kwa upande wake, Ally Shomari amebainisha kuwa chama hicho kina wanachama wengi wakulima ambao mfumo wa elimu waliyosoma enzi zao haulingani na sasa, kwa hiyo, TCCIA Pwani itoke ilipokua zamani kutumia kingereza ianze kutumia lugha ya Kiswahili ili kurahisisha mawasiliano.
Naye msimamizi wa uchaguzi huo, Joseph Kahungwa ambaye pia ni Makamu wa Rais wa TCCIA Taifa upande wa kilimo, amebainisha kuwa uchaguzi unafanyika baada ya uongozi uliokuwepo kuvunjwa mapema Januari mwaka huu na halmashauri kuu Taifa ya chama hicho kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo kuvunja katiba ya umoja huo.

No comments:
Post a Comment