Na John Walter-Manyara
Naibu waziri wa Mifugo na Uvuvi Paulina Gekul amewataka maafisa Ugani kumsaidia Rais Dr. John Pombe Magufuli katika kutimiza adhma yake ya kuwasaidia wafugaji nchini kufikia ufugaji wa kisasa wenye tija ili kuchagia ukuaji wa Viwanda.
Gekul ameyasema hayo Mjini Babati mkoa wa Manyara wakati akifungua kikao kazi cha kuwajengea uwezo maafisa Ugani kutoka mikoa ya Kanda ya kaskazini.
Amesema wafugaji wakipata maarifa mapya na huduma bora za ugani, zitachochea ongezeko la uzalishaji wa malighafi zitokanazo na mifugo kwa ajili ya uchumi wa Viwanda.
Gekul amesema Sekta ya Mifugo na Uvuvi inachangia katika kuwapatia wananchi ajira, Chakula, lishe, kipato na fedha za kigeni.
"Sekta hii ni sekta ambayo kuanzia asubuhi mpaka jioni kila Mtanzania anashiriki, asiposhiriki kwa maziwa atashiriki kwa nyama, asiposhiriki kwa nyama ya Ngo'mbe atashiriki kwa nyama ya Kuku, asipochoma nyama atakunywa supu, na asipotumia mazao ya mifugo atatumia samaki, kwa hiyo ni sekta ambayo kuanzia asubuhi mpaka jioni inagusa maisha ya kila Mtanzania" Paulina Gekul Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi.
Aidha ameeleza kuwa mbali ya kuwa wizara ya Mifugo na Uvuvi inachangia asilimia 7.4 ya pato la taifa lakini bado hawaridhishwi na mchango wa sekta hiyo ukilinganisha na sekta zingine hivyo ni matarajio yao makubwa baada ya wataalamu hao kujengewa uwezo, itasaidia kuongeza pato kwa taifa.
Amesema ukuaji wa sekta hiyo kwa miaka kadhaa iliyopita ilikuwa asilimia 4.9 na sasa imefikia asilimia 5 kwa mujibu wa takwimu za mwaka 2019/2020 huku wakiwa na mpango wa kuongeza ukuaji huo kupitia mafunzo wanayoyatoa kwa maafisa Ugani katika kanda zote nchini.
Amesema takwimu ya rasilimali Mifugo iliyopo nchini inakadiriwa kuwa kuna Ng'ombe milioni 33.4, Mbuzi 21.29, Kondoo Milioni 5.65, Kuku wa asili Milioni 38.77, Kuku wa Kisasa Milioni 44.51, Nguruwe Milioni 2.14 na punda wapatao Laki 659,389.
Amesema inawezekana Takwimu hizo za wizara wanazozitumia kwa sasa zikawa zimeongezeka au zimepungua huku mikoa nayo ikiwa na takwimu zake ambazo wizara imedhamiria kuziboresha.
Kwa upande mwingie Naibu waziri wa Mifugo na Uvuvi amesema kwa sasa nchi inazalisha Tani laki 7.1 za nyama lakini zinazosafirishwa kwenda nje ya nchi hazizidi Tani Mia sita.
No comments:
Post a Comment