Gavana wa zamani wa Benki Kuu ya Ulaya (ECB) Mario Draghi ataapishwa leo na kuanza kutumikia wadhfa wake mpya kama waziri mkuu wa Italia.
Draghi ameridhia kuchukua nafasi hiyo ya kuiongoza serikali mpya ya umoja baada ya kukutana na Rais wa Italia Sergio Mattarella jana Ijumaa hali ambayo imeufikisha mwisho mzozo wa kisiasa uliokuwepo kwa zaidi ya wiki nne nchini humo.
Mwanauchumi huyo mwenye umri wa miaka 73 aliwasilisha mbele ya waandishi wa habari orodha yake ya mawaziri, yenye idadi zaidi ya wanasiasa na pia wataalam kadhaa ambao sio wanasiasa.
Kwenye orodha hiyo Luigi Di Maio atabaki kuwa waziri wa mambo ya nje na Roberto Speranza ataendelea na wadhfa wake wa waziri wa afya, hatua hiyo inamaanisha kwamba baadhi ya mawaziri waliokuwepo wakati wa utawala wa waziri mkuu wa zamani Giuseppe Conte wataendelea kuhudumu katika baraza jipya la mawaziri.
Draghi sasa anahitaji kushinda katika kura ya kuwa na imani naye katika mabunge yote mawili nchini Italia ili kuithibisha serikali yake.

No comments:
Post a Comment