Search This Blog

Sunday, February 14, 2021

Diana Madukwa awataka TARURA kutokukaa maofisini bali waende 'field' kucheki hali za barabara


KAIMU Katibu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Dodoma Mjini, Diana Madukwa amelitaka Jiji la Dodoma kumchukulia hatua za kinidhamu Mkandarasi aliyepewa dhamana ya kutengeneza Barabara inayotoka eneo la Ihumwa kwenda Kikombo kutokana na mkandarasi huyo kusuasua na ujenzi.

Madukwa amelitoa agizo hilo kwenye ziara ya Kamati ya Siasa Wilaya ya Dodoma Mjini ya kukagua miundombinu ya Jiji hilo ambayo pia alitumia fursa hiyo kuwakumbusha viongozi wa serikali jukumu la kusimamia miradi ya miundombinu inayotekelezwa kwa wivu wa kizalendo kama ambavyo Rais Dk John Magufuli amekua akifanya.

Amemuagiza pia Meneja wa Wakala wa Barabara Mjini na Vijijini (TARURA) kuwa na utaratibu wa kukarabati barabara kwa wakati siyo kusubiri mpaka wananchi wailalamikie serikali ndipo na wao wajitokeze kuanza kufanyia matengenezo miundombinu hiyo ili wananchi wasipate shida.

" Kwanza huyu mkandarasi wa hii barabara ya Ihumwa kwenda Kikombo ni wa kumchukulia hatua kali sana, haiwezekani tenda alipewa na Jiji toka Desemba mwaka jana halafu alichofanya ni kuleta mashine zake hapa bila kuanza ujenzi, nilitake Jiji kuanza kumfuatilia na ikiwezekana achukulie hatua , kinidhamu, kwanini turuhusu wananchi wetu wapate shida wakati tulishampa mkandarasi tenda?.

TARURA mnafanya kazi nzuri lakini pia jiwekeeni utaratibu wa kutoka kwenda field kuangalia miundombinu yetu, ni ajabu kuona nyie mpoa lakini wananchi bado wanalalamika barabara fulani mbovu na nyie hamuijui, hii inaonesha jinsi gani hamtoki maofisini kuja mitaani kuangalia hali ilivyo, achieni viti hivyo tokeni mkakague barabara, " Amesema Madukwa.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Dodoma Mjini, Meja Mstaafu Johnick Risasi amewataka TARURA kuhakikisha wanatengeneza barabara zote zenye changamoto ili wananchi waweze kupita kwani zimekua zikikwamisha shughuli nyingi za kimaendeleo na kuinyima serikali mapato pamoja na wananchi kukosa mapato yao.

Kamati hiyo ya Siasa imefanya ziara katika Kata za Ihumwa, Kilimani, Nzuguni na Uwanja wa Ndege na kujionea namna ambavyo barabara zimeharibika na kuzitaka mamlaka zinazohusika kutekeleza maagizo hayo kwa haraka ili kutoa huduma kwa wananchi ambao walichagua CCM kwa kishindo katika uchaguzi mkuu uliopita.



No comments:

Post a Comment

Punguza kilo tano kwa siku saba

  NI watu wachache wanaopenda kunenepa, wengi wanapenda miili ya wastani kwa kuwa  unene si mzuri. Ukiwa mnene si tu kwamba unakaribisha m...