Balozi wa Israel nchini Marekani Gilad Erdan, amesema jana kuwa waziri wake mkuu Benjamin Netanyahu hana wasiwasi wowote kwamba rais wa Marekani Joe Biden hajampigia simu huku akionekana kujaribu kupuuza ukosefu huo wa mawasiliano ya moja kwa moja kufikia sasa.
Erdan amesema kuwa Netanyahu hana wasiwasi kuhusu wakati wa mazungumzo na kwamba Biden ana masuala muhimu ya kushughulikia kama vile janga la virusi vya corona na kudorora kwa uchumi.
Siku ya Ijumaa ikulu ya White House ilikanusha kwamba Biden alikuwa anampuuza Netanyahu kimaksudi kwa kukosa kumjumuisha katika mawasiliano ya simu na viongozi wa kigeni kufikia sasa tangu alipochukuwa hatamu za uongozi mnamo Januari 20 na kusema viongozi hao wawili watazungumza karibuni.
Kumekuwa na uvumi kwamba Biden anaonyesha ishara ya kutoridhishwa na uhusiano wa karibu aliokuwa nao Netanyahu na rais wa zamani Donald Trump, aliyempigia simu siku mbili baada ya kuapishwa kwake mnamo mwaka 2017.

No comments:
Post a Comment