Mapigano ya kikabila katika mkoa wa Darfur nchini Sudan jana yalisababisha vifo vya watu wawili na kuteketezwa kwa majengo kadhaa katika ghasia za hivi karibuni zilizotokea katika eneo hilo la mashambani.
Shirika la habari la serikali nchini humo SUNA, limeripoti kuwa mapigano hayo yalitokana na mzozo kati ya jamaa ya makabila tofauti katika mji mkuu wa El Geneina wa jimbo la Darfur Magharibi.
Haikubainika mara moja kilichosababisha malumbano hayo.
Shirika la SUNA limeongeza kuwa gavana wa jimbo hilo la Darfur Magharibi alitoa uamuzi wa maafisa wa usalama kutumia nguvu kutuliza hali katika eneo hilo la El Geneina.
Hata hivyo, chama cha mawakili katika eneo la Darfur na kundi moja la asasi ya kijamii katika eneo hilo, yamesema kuwa makundi ya kujihami yalitumia fursa hiyo kuchochea zaidi ghasia hizo.
Shirika la SUNA limeripoti kuwa waziri mkuu Abdalla Hamdok ameagiza ujumbe wa maafisa wakuu kutumwa katika eneo la Darfur Magharibi kufuatilia hali ilivyo.

No comments:
Post a Comment