Na John Walter-Manyara.
Mwenyekiti mstaafu wa kijiji cha Kimotorok, Merubo Parimelo na mjumbe mstaafu wa serikali ya kijiji hicho Daniel Melau wanashikiliwa na TAKUKURU wilayani Simanjiro mkoani Manyara kwa tuhuma mbalimbali.
Taarifa iliyotolewa na mkuu wa Taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa mkoa wa Manyara Holle Makungu imesema kuwa. wawili hao wanatuhumiwa kughushi na kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.
Makungu amesema wakati viongozi hao wastaafu wakipekuliwa, wamekutwa na nyaraka za serikali ambazo wamekuwa wakizitumia kuuza ardhi ya kijiji kwa kurudisha tarehe nyuma ili kuonyesha mauzo hayo yalifanyika wakiwa madarakani.
Amesema uchunguzi zaidi unaonyesha kuwa baadhi ya wenyeviti wastaafu wa vijiji katika wilaya ya Simanjiro huondoka na nyaraka za serikali za vijiji kwa nia ya kutenda uhalifu wa kuuza ardhi japokuwa hawapo kwenye uongozi.
Makungu amewataka viongozi walioondoka madarakani na nyaraka za serikali kuzirejesha na kuzikabidhi kwa watendaji wa vijiji vinavyohusika kwani wasipofanya hivyo watakutana na mkono wa sheria.

No comments:
Post a Comment