Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika zimekamilisha ujumbe wake wa kulinda amani katika jimbo la Darfur nchini Sudan. Ujumbe wa kudumisha amani umefikia mwisho baada ya kuwepo katika eneo hilo lililokumbwa na migogoro kwa muda wa miaka 13.
Umoja wa mataifa umesema hatua hiyo inatekeleza azimio la Baraza la Usalama lililofikiwa mnamo Desemba 22 mwaka jana.
Kufikia ukomo wa ujumbe huo wa Umoja wa Mataifa UNAMID, kunamaanisha jukumu la ulinzi wa raia limehamishiwa kwa serikali ya Sudan.
Hata hivyo wanaharakati wa kutetea haki za binadamu wameikosoa hatua hiyo kutokana na kuwa hali ya usalama bado ni ya wasiwasi katika jimbo la Darfur. Zoezi la kuondoka askari hao wa Umoja wa Mataifa wapatao 16,000 linatarajiwa kukamilika mnamo Juni 30.
Msemaji wa UNAMID Ashraf Eissa amesema ujumbe wa kisiasa wa Umoja wa Mataifa UNITAMS utakaosaidia kipindi cha mpito nchini Sudan utawekwa katika jimbo la Darfur baada ya UNAMID kuondoka.

No comments:
Post a Comment