Polisi nchini Tunisia wamewakamata watu zaidi ya 600 katika maandamano yenye vurugu yalioingia siku ya nne.
Siku ya Jumatatu, vijana wengi waliokuwa wameandamana walikusanyika tena katikati ya mji wa Tunis, wakirushia polisi mawe na mabomu ya petroli.
Vikosi vya usalama vilijibu kwa kurusha mabomu ya machozi na maji ya kuwasha.
Tunisia inakabiliwa na changamoto za kiuchumi na theluthi moja ya vijana nchini humo hawana kazi.
Mgogoro wa kiuchumi umeendelea kuzorota kwasababu ya janga la corona.
Maandamano ya hivi karibuni yanafanyika ikiwa ni miaka 10 tangu kutokea kwa mapinduzi nchini Tunisia yaliodai demokrasia na kusababisha vuguvugu la maandamano katika mataifa ya Kiarabu.
Hatahivyo, matumaini kuwa maandamano haya yataleta ajira yamefifia.
Nje ya mji wa Tunis, kumeripotiwa ghasia Jumatatu katika miji ya Kasserine, Gafsa, Sousse na Monastir.
Msemaji wa wizara ya mambo ya ndani amesema idadi kubwa ya waliokamatwa tangu kutokea kwa maandamano hayo Ijumaa, ni wenye umri mdogo ambao wamekamatwa kwa makosa ya kusababisha uharibifu na uporaji.
Khaled Hayouni alisema maafisa wawili wa polisi wamejeruhiwa.
"Hilo halinauhusiano wowote na maandamano yanayoruhusiwa kisheria na kikatiba," Bwana Hayouni amesema. "Maandamano yanafanyika mchana... bila kutokea kwa vitendo vyovyote vya kiuhalifu ."

No comments:
Post a Comment