Waziri wa Utalii nchini Kenya Najib Balala ametetea uamuzi wa kumtaja mwanamitindo wa Uingereza Naomi Campbell kuwa balozi wa utalii kimataifa kwa nchi hiyo.
Wakati wa hafla ya umma, Bwana Balala alisema anajua Wakenya wengi wameuliza kwanini muigizaji wa Hollywood Lupita Nyong'o hakuchaguliwa katika nafasi hiyo.
Waziri akajibu kwamba wamekuwa wakimtafuta Bi. Nyong'o lakini hajapatikana kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita.
Muigizaji huyo wa Kenya ambaye pia ni mshindi wa tuzo ya Oscar alipendekezwa na Wakenya katika mitandao ya kijamii kuwa mtu sahihi wa kushikilia nafasi ya balozi wa utalii kimataifa kuwakilisha Kenya.
Bwana Balala alisema Bi. Campbell amechukua nafasi hiyo kwa maslahi ya umma na kwamba serikali inafanyia kazi namna ya kutumia ushawishi wake kutangaza utalii, kulingana na vyombo vya habari vya nchini Kenya.

No comments:
Post a Comment