Rais wa Marekani Joe Biden amezungumza na mwenzake wa Ufaransa Emmanuel Macron jana Jumapili na kuahidi kufanya kazi kwa karibu kupambana na janga la virusi vya corona, mabadiliko ya tabia nchi na kuufufua tena uchumi wa dunia.
Taarifa iliyotolewa na ikulu ya Marekani imesema Biden pia amezungumzia azma yake ya kuimarisha ushirika wa mataifa ya magharibi kupitia Jumuiya ya Kujihami ya NATO na mahusiano ya karibu na Umoja wa Ulaya.
Kadhalika viongozi hao wawili wamekubaliana kushirikiana kwenye masuala yanayohusu China, Mashariki ya Kati, Urusi na kanda ya Sahel barani Afrika inayoandamwa na mashambulizi ya makundi ya itikadi kali.
Hayo yalikuwa mazungumzo ya kwanza kati ya Macron na Biden ambaye wiki iliyopita aliapishwa kuingoza Marekani na kuhitimisha enzi ya Donald Trump ambaye utawala wake ulidhoofisha mahusiano ya Washington na Paris.

No comments:
Post a Comment