Mjumbe wa bodi ya kampuni ya madini ya Twiga, Casmir Kyuki amedokeza kuwapo kwa matumaini ya Serikali ya Tanzania kulipwa deni lake la Dola200 milioni ( sawa na Sh463 bilioni) ambazo inaidai kampuni ya Barrick, ikiwa mwenendo wa soko la dhahabu duniani utaendelea kuwa mzuri kama ulivyo sasa.
Fedha hizo ni sehemu ya Dola 300 milioni (Sh695 bilioni) ambazo Barrick iliahidi kuzilipa kama fidia, kutokana na kampuni yake tanzu ya Acacia kudaiwa kodi na tozo mbalimbali na mamlaka za serikali ya Tanzania
Malipo ya fedha hizi zilikuwa miongoni mwa makubaliano kati ya Kampuni ya Barrick na Serikali ya Tanzania ya uendeshaji wa shughuli za madini yaliyosainiwa Julai, 2019 na baadae kuanzishwa kwa kampuni ya madini ya Twiga, Oktoba, 2019.
Kampuni ya Barrick ilishatoa kiasi cha Dola100 milioni (Sh231 bilioni), ambapo kiasi cha Dola200 milioni inatakiwa kuzilipa katika miaka minne ijayo.
Kyuki na Rais wa Barrick, Mark Bristow juzi walizungumza na waandishi wa habari kwenye mgodi wa Bulyanhulu ulioko mkoani Shinyanga na kueleza mafanikio ya mwaka mmoja ya uendeshaji wa pamoja wa migodi ya dhahabu kwa ubia chini ya kampuni ya Twiga.
Alisema katika kipindi hicho kumekuwa na mafanikio makubwa katika mwaka uliopita hasa ikichangiwa zaidi na bei nzuri ya dhahabu kwenye soka la dunia,
Aligusia kitendo cha kulipwa kwa kodi na tozo mbalimbali za Serikali na kutolewa kwa gawio kama makubaliano ya uanzishwaji yanavyoelekeza, kunaashiria mwelekeo mzuri.
Kyuki alisema kutokana na mwenendo huo mzuri wa kimapato, kuna uwezekano kwa Barrick kukamilisha deni lao mapema hata kabla ya wakati uliopangwa.
“Unajua Twiga imeleta ufanisi mkubwa katika uendeshaji wa sekta ya dhahabu, na katika mwaka mmoja uliopita kodi, tozo na gawio vimelipwa,’’alisema.
Imeandikwa na Samson Mfalila, Mwananchi Mwananchipapers@mwananchi.co.tz

No comments:
Post a Comment