Na Faruku Ngonyani , Mtwara
Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Manispaa ya Mtwara-Mikindani lililoketi hii leo Januari 29,2020 limepitisha rasimu ya Mpango wa bajeti ya mwaka wa fedha 2021/22 yenye jumla ya shilingi 27,745,580,924.38.
Awali akiwasilisha rasimu hiyo Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Mtwara-Mikindani Bwana Gryson Orcado amesema kuwa katika rasimu ya bajeti iliyopitishwa Manispaa imekadiria kukusanya Shilingi 4,950,000,000 kutoka katika mapato ya ndani ambayo imeongezeka kutoka shilingi 4,930,000,000 iliyopangwa kukusanya katika bajeti inayotekelezwa sasa.
Pamoja na chanzo hiko pia Manispaa inakadiria kukusanya Shilingi 787,816,000 kutoka Serikali kuu kama ruzuku ya matumizi ya Kawaida, shilingi 16,980,752,000 ruzuku ya mishahara na 5,027,012,924.38 ruzuku ya Miradi ya Maendeleo
Kwa upande wa matumizi Orcado amesema kuwa Manispaa inatarajia kutumia shilingi 27,745,580,924.38 kutekeleza Miradi ya Maendeleo, kulipa mishahara na Matumizi ya Kawaida.
Aidha katika bajeti hiyo Manispaa inatarajia kutumia shilingi 2,144,451,750 kutoka katika mapato yake ya ndani kutekeleza Miradi ya Maendeleo.
Maandalizi ya bajeti ya mwaka ujao imezingatia vigezo mbalimbali vikiwemo Ilani ya Uchaguzi ya Chama Tawala mwaka ya 2020/2025, Vipaumbele mbele cha wananchi vilivyotokana na jitihada za jamii, sheria ya bajeti No. 11 ya mwaka 2015, ahadi za viongozi mbalimbali wa Serikali, Mpango Mkakati wa halmashauri wa mwaka 2018/19-2022/23, wasifu wa halmashauri wa mwaka 2017 pamoja na vigezo Vingine vilivyowekwa na Serikali.

No comments:
Post a Comment