Search This Blog

Saturday, January 30, 2021

Askofu Shoo amvaa meya aliyewavua watu barakoa

 


Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Askofu Fredrick Shoo ameeleza kusikitishwa na kitendo cha Meya wa Manispaa ya Moshi, Juma Raibu kuwaamuru wananchi waliokuwa katika kikao cha Baraza la Madiwani kuvua barakoa.


Askofu Shoo, ambaye pia ni mkuu wa Dayosisi ya Kaskazini ya kanisa hilo, alisema kitendo cha meya huyo kuwalazimisha wananchi wanne kuvua barakoa ni kukosa hekima na uwajibikaji wa kiwango cha juu kama kiongozi wa kisiasa.


“Itoshe tu kusema nimesikitishwa sana na kitendo cha huyu meya, kuwalazimisha watu kuvua barakoa, ni kukosa hekina na uwajibikaji kwa kiwango cha juu,” alisema Askofu Shoo na kusisitiza umuhimu wa kuendelea kujikinga.


“Kuna barua nimesaini iende kwa viongozi na washarika wote wa KKKT. Kutokuchukua tahadhari ni sawa na kumjaribu Mungu. Kuchukua tahadhari ni wajibu si upungufu wa imani na si dhambi wala si kosa la jinai.


“Tusitawaliwe na hofu, bali tuzidi kumuomba Mungu na kuchukua tahadhari za kujikinga na kuzuia maambukizi kama tulivyofanya wakati ugonjwa ulipolipuka,” alieleza. Ugonjwa wa corona uliingia nchini kwa mara ya kwanza Machi, mwaka jana.


Akizungumza katika kikao cha Baraza la Madiwani maalumu kwa ajili ya kupitisha bajeti ya Halmashauri hiyo, Meya huyo aliwasimamisha wananchi wanne waliokuwa wamevaa barakoa na kuwamuru wazivue.


Uvaaji wa barakoa, ni moja kati ya njia zinazoelekezwa na wataalamu wa afya hapa nchini na Shirika la Afya Duniani (WHO), kwa ajili ya kujikinga na kusambaa kwa ugonjwa wa homa kali ya mapafu inayosababishwa na virusi vya corona.


Kabla ya kuanza kikao hicho juzi, Meya huyo alisema “Kuna kitu nimekiona hapa (ukumbini) hakijanifurahisha kabisa. Nyie mliovaa barakoa simameni. Nyie mliovaa barakoa, vueni barakoa zenu. Vueni barakoa tuko sehemu salama.


“Nitumie nafasi hii kuwakaribisha kwenye kikao. Manispaa iko shwari. Hayo mabarakoa yenu mnayoyavaa hayo hali iko shwari. Yaani nyie mliovaa ndio mnajipenda zaidi na akivaa mwingine askari mumtoe nje,” alisema Meya huyo.


Kana kwamba hiyo haikutosha, baada ya kumaliza kikao na kutafutwa na wanahabari ili afanunue amri yake hiyo, Meya Raibu, alishikilia msimamo wake huo akisema amefanya hivyo kwani uvaaji barakoa ni kuwatia hofu wananchi.


“Corona ipo tunaweza kujikinga lakini manispaa ya Moshi haina corona na ndio maana nikawaambia vueni barakoa na msikilize kikao kama ambavyo tunaamini kwamba tunapaswa kujikinga lakini tusitiane hofu,” alisema Meya huyo.


“Na ninaendelea kuwaelekeza katika eneo la langu la Manispaa sitaruhusu mtu yeyote aingie na barakoa katika kikao changu kwani tunaamini tuko salama salmini,” alisisitiza meya huyo ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Bomambuzi CCM.


Kauli ya meya huyo ilikuja siku moja tu baada ya Rais John Magufuli akiwataka Watanzania.


Tuendelee kumtanguliza Mungu wetu huku tukichukua tahadhari za kiafya kadri tutakavyokuwa tunaambiwa na wataalamu wetu lakini tujihadhari sana,” alisema Rais Magufuli alipokuwa akizindua shamba la miti la Silayo lililopo Chato.


Rais Magufuli aliwataka Watanzania kuendelea kuchukua tahadhari zingine za kiafya ikiwa ni pamoja na kujifukizia, akisema “Unajifukizia huku unamuomba Mungu unasali, unaswali.”


Aliongeza, “huku unapiga zoezi la kufanya la kulima mahindi la kulima viazi ili ule vizuri ushibe ili corona ashindwe kuingia kwenye mwili wako. Mtatishwa sana ndugu zangu Watanzania lakini simameni imara.”


“Ninajua wako baadhi ya Watanzania hata wameondoka ndani ya nchi na kukimbilia maeneo mengine na kwenda kuchanjwa na walikochanjwa huko wamekuja huku (Tanzania) wametuletea corona ambayo ni ya ajabu ajabu”


Rais Magufuli aliitaka wizara ya afya kuwa makini na chanzo hizo akisema nyingine hazifai na kuitaka kuacha kukimbilia chanjo na sio kila chanjo ni ya maana kwa taifa la Tanzania akisema baadhi ya chanjo zina madhara.



No comments:

Post a Comment

Punguza kilo tano kwa siku saba

  NI watu wachache wanaopenda kunenepa, wengi wanapenda miili ya wastani kwa kuwa  unene si mzuri. Ukiwa mnene si tu kwamba unakaribisha m...