Search This Blog

Monday, December 28, 2020

Ndugulile Aipa TCRA Miezi Mitatu Kumaliza Changamoto Za Vifurushi Na Bando Kwa Wananchi


Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt.Faustine Ndugulile ameipa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) miezi mitatu kumaliza changamoto za bando na vifurushi zinazotolewa na kampuni za simu za mkononi kwa wananchi


Dkt. Ndugulile ameyasema hayo wakati wa ziara yake alipotembelea TCRA ikiwa ni moja ya taasisi zilizo chini ya Wizara hiyo kwa lengo la kufahamiana, kutambua majukumu yao na kuzungumza na Bodi, Menejimenti na wafanyakazi wa taasisi hiyo ili kuwa na uelewa wa pamoja na kushirikiana kwa kufanya kazi kwa pamoja katika kuhudumia wananchi kuelekea Mapinduzi ya Nne ya Viwanda na kuiwezesha Tanzania kuwa na uchumi wa kidijitali


Ameongeza kuwa TCRA ishughulikie malalamiko ya wananchi kwa kuwa wananchi hawana imani na vifurushi na bando, na kuwe na mfumo wa kuhakiki gharama halisi za mawasiliano kuendana na fedha aliyotoa mwananchi na kuwe na namba ya bure ambayo wananchi watapiga ili kuwasilisha malalamiko yao ili kuwawezesha wananchi kuongeza imani yao kwa Serikali


Amesisitiza kuwa ni heri tufanye maamuzi mabaya kuliko kutokufanya maamuzi na amewataka washirikiane na Baraza la Watumiaji wa Huduma za Mawasiliano (TCRA – CCC) kumaliza changamoto hiyo kwa kuwa watanzania sio wajinga, anataka aone kapata shilingi moja anaitumia shilingi moja yake kupiga simu


Pia, amehimiza wahakikishe kuwa chaneli tano za bure za runinga zinaonekana hata baada ya muda wa kulipia kumalizika kwa kuwa chaneli hizo hazionekani kwenye baadhi ya ving’amuzi  


Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Mhandisi Kundo A. Mathew ameipongeza TCRA kwa kutengeneza mifumo ya TEHAMA, kutambua changamoto zilizopo na imejipanga kuzifanyia kazi kwa kuwa lazima TEHAMA ichukue nafasi yake na itufikishe watanzania tunakotaka kwenda


Naye Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt.Zainab Chaula amewataka wafanyakazi wa TCRA kujiongeza na kujituma zaidi badala ya kusubiri maagizo na maelekezo kwa kuwa wao ni wataalamu, hivyo washirikiane kwa pamoja ili kuhakikisha kuwa wanaendelea kuwahudumia watoa huduma na watumiaji wa huduma za mawasiliano


Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, Mhandisi James Kilaba amekiri uwepo wa changamoto za bando na vifurushi na ameahidi kuzifanyia kazi kwa kuwa TEHAMA imeongeza mnyororo wa thamani kwenye sekta zote na imesogeza huduma mbali mbali viganjani



No comments:

Post a Comment

Punguza kilo tano kwa siku saba

  NI watu wachache wanaopenda kunenepa, wengi wanapenda miili ya wastani kwa kuwa  unene si mzuri. Ukiwa mnene si tu kwamba unakaribisha m...