Na Omary Mngindo, Mlandizi
MBUNGE wa Jimbo la Kibaha Vijijini Mkoa wa Pwani Michael Mwakamo, amesema kuwa anatamani Halmashauri ya Kibaha (Kibaha Vijijini) iwe na Chama Cha Mpira wa Miguu kitachojitegemea.
Mwakamo alitoa rai hiyo mjini hapa akizungumza na Waandishi wa Habari, ambapo alisema kuwa pamoja na kwamba Kibaha ina chama chake KIBAFA, lakini ina majimbo mawili hivyo kuwanyima fursa vijana waliopo pembezoni mwa miji kuonesha vipaji vyao.
Alisema kuwa Halmashauri yake ina Vijiji vinavyounda Kata za Kikongo na Dutumi zinapakana na Kisarawe, Magindu inapakana na Morogoro Vijijini, huku Kata ya Gwata ikipakana na wilaya ya Bagamoyo hivyo kutokana na jiografia inakuwa vigumu kushiriki ligi kutokana na hali ya kiuchumi.
"Kwakuwa lengo kubwa ni kucheza mpira, basi niwaombe wenye dhamana wapunguze baadhi ya vigezo vinavyoukwamisha mchezo huo, tukumbuke kwamba Rais wetu Dkt. John Magufuli pamoja na kukabiliwa na majukumu mengi, pia anauangalia mchezo huu hivyo tumsaidieni," alisema Mwakamo.
Alisema kuwa hivi karibuni Rais aliizungumzia timu ya Taifa (Taifa Star's), akionesha kukerwa kutokana na kutokuwepo kwa matokeo mazuri, hali inayomuumiza sana, huku akiongeza kuwa anatambua fika kuwa mchezo huo unasimamiwa na Katiba, Kanuni na Sheria.
"Natambua kwamba kitu chochote kinasimamiwa na taratibu zake, lakini upande wa soka hivyo sio Msaafu ambao hauwezi kufanyiwa maboresho, tuangalie vinavyokwamisha tuvipunguze ili mpira uchezwe, tupate wachezaji wazuri wa pembezoni mwa miji," aliongeza Mbunge huyo.
Aidha Mwakamo aligusia ukubwa wa Halmashauri ya Chalinze wilaya ya Bagamoyo, ambayo ina vijiji na vitongoji vinavyopakana na Wilaya za Handeni Tanga, Mvomero na Mikese vya Mkoa wa Mrogoro vyote vinategemea BFA ambayo Makao yake Makuu yapo Bagamoyo mjini.
"Hiyo ni picha kwa ufupi tu ambayo tunayo wana-Pwani sijagusia wilaya nyingi ambazo nazo zinakabiliana na changamoyo kama hizi, niwaombe viongozi tuliopatiwa dhamana ya kuusimamia mpira tumsaidie Rais wetu kwani anaguswa na maendeleo ya mchezo huu," alisema Mwakamo.
Alisema kuwa maeneo mengi jimboni humo kuna mashindano ya Ndondo yanayoandaliwa na wadau ya kuwania zawadi mbalimbali, ambayo hayavipatii fursa vilabu husika kushiriki ligi yeyote, hivyo kutowapatia nafasi vijana kuonekana nje ya maeneo yao.
No comments:
Post a Comment