Na Omary Mngindo, Mlandizi
TAASISI ya MAMAUKI inayojihusisha na Maendeleo ya Makazi, Uchumi na Kilimo kwa wakazi wa Mlandizi Kibaha Pwani, inaiomba Serikali kuruhusu madarasa ya kidato cha kwanza mpaka nne shule ya Sekondari ya Wasichana Ruvu yatumike.
Vyumba hivyo kuanzia kidato cha kwanza mpaka cha nne katika shule hiyo ambayo kwa sasa ina kidato cha tano na sita, pamoja na kuwa na madawati ya kutosha lakini havitumiki, huku wanafunzi wengi wakipangiwa shule za mbali.
Hayo yamebainishwa na Mwenyekiti wa taasisi hiyo Dick Simba akizungumza na Waandishi wa habari mjini hapa, ambapo alisema taasisi yao imefanya utafiti wa kina katika nyanja mbalimbali wakishirikiana na wananchi, kisha kujiridhisha kuwepo kwa vyumba hivyo shuleni hapo.
"MAMAUKI tumefanya utafiti wa kina, tumebaini kuna vyumba vilivyotumika kwa kidato cha kwanza mpaka cha nne, kwa sasa havitumiki kutokana na shule kuwa ya kidato cha tano na sita, tunaiomba serikali iviruhusu ili wataoanza kidato cha kwanza wavitumie," alisema Simba.
Alisema kuwa wanapaza sauti kwa lengo la kuwasaidia wazazi na kwamba mwaka 2020 shule za msingi Mlandizi wamefaulisha wanafunzi wengi, hivyo kupangiwa shule za Soga, Kwala na Magindu ambapo kuna umbali usiopungua kilometa 15, 20 na 40 hali adha kwa wazazi.
"Hali hiyo ni mtihani mkubwa kwa wazazi na walezi ambao wana hali tete kiuchumi, pia kwa wanafunzi kitaaluma wanakuwa na changamoto kubwa, kiilio hiki ni cha muda mrefu, tunaiomba Serikali iruhusu kidato cha kwanza mpaka nne wasome Ruvu," alisema Mwenyekiti hiyo.
Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti Selemani Pazi alisema kwamba katika kukabiliana na changamoto hiyo, wanawaomba wananchi kwa kusaidiana na wadau wa elimu kuhamasishana kujenga vyumba vipya vya madarasa vitavyoondoa adha hiyo.
"Sisi MAMAUKI kazi yetu kusimamia Maendeleo ya Makazi, Uchumi na Kilimo kwa wakazi wa Mlandizi ikiwemo sekta za elimu, afya na nyinginezo, tunaiomba serikali tushirikiane na wadau kujenga shule za kutosha ili kukabiliana na upungufu huo," alisema Pazi.

No comments:
Post a Comment