Na John Walter-Manyara
Maandalizi ya Mashindano ya Netiboli (TAIFA CUP) ambayo yanatarajiiwa kufanyika kitaifa mkoa wa Manyara Januari 3,2021 katika mji wa Babati yanendelea kushika kasi.
Kamati ya maandalizi ya Mashindano hayo inaeleza kuwa imejipanga vizuri kuwapokea wageni watakaowasili kutoka mikoa mbalimbali.
Kwa upande wa timu ya mkoa wa Manyara inayosimamiwa na Katibu wa Chama cha Netiboli mkoa wa Manyara Bi. Yasinta Sylivester ambaye pia ni Mjumbe wa CHANETA Taifa, amesema wanaendelea kujiweka sawa kwa kucheza mechi mbalimbali za kirafiki.
Sylivester ameomba ushirikiano kutoka kwa wakazi wa mkoa wa Manyara na wadau wa soka kuelekea mashindano hayo ya kitaifa.
Amesema kuwa maandalizi yapo vizuri na kwamba timu inaendelea na mazoezi kukabiliana na wapinzani watakaokutana nao.
Hivi karibuni katika kikao cha Kamati ya ushauri ya mkoa (RCC) mkuu wa mkoa wa Manyara Joseph Joseph Mkirikiti alisema ni fursa kwa mkoa huo kuchaguliwa kuwa mwenyeji wa Mashindano hayo kwani licha ya kuutangaza mkoa lakini pia itakuza uchumi wa mkoa.
Wakiwa Dareda kati kata ya Ayalagaya kwenye mchezo wa Kirafiki na wanafunzi wa Shule ya Sekondari Ayalagaya, Mwalimu Mkuu msaidizi wa shule hiyo Gordian Thomas, amewataka wachezaji hao wajitume kwa kuwa michezo ni ajira.
Diwani wa kata ya Ayalagaya Mheshimiwa Sabini John, amesema mchezo huo wa kirafiki ni heshima kwao kwa kuwa uwanja wa shule ya Sekondari Ayalagaya ulitangazwa kuwa wa Kanda na aliyekuwa waziri wa Habari,Utamaduni sanaa na Michezo Dr. Harrison Mwakyembe pindi alipofika eneo hilo.
Aidha amepongeza uongozi wa Chama cha Netiboli Tanzania (CHANETA) Kwa kukubali mashindano ya Taifa Cup yafanyike Kitaifa katika mkoa huo kwa kuwa ni fursa ya kukuza uchumi na kuutangaza mkoa huo.
Padri Laurence Lawala wa Ayalagaya akiwakaribisha wachezaji wa timu ya mkoa wa Manyara kwenye mchezo huo wa kirafiki dhidi ya wanafunzi wa Sekondari Ayalagaya, amesema kila mmoja ashiriki mashindano hayo kwa nia njema ya kudumisha upendo, amani na mshikamano.
Amesema kila anayeshiriki mashindano hayo ajitambue kwamba anatekeleza wajibu muhimu wa kudumisha ushirikiano kati ya maeneo wanayotoka na kujenga afya yake binafsi na kuwavuta wengine waweze kushiriki kwenye michezo.
Amewataka wachezaji wacheze kwa upendo na amani na kujaliana wakitambua kwamba wao ni wa taifa moja, jamii moja, binadamu ambao wameumbwa kwa sura na mfano wa Mwenyezi Mungu hivyo ni vyema kushirikiana ili Mungu awape baraka zake.
Naye Baba Paroko Joseph Bukhay amewapa moyo Vijana wa Timu ya Netiboli mkoa wa Manya kwa kuwaeleza kuwa michezo ni afya,hudumisha undugu,umoja,urafiki lakini pia Michezo ni ajira hivyo vijana wajitume.
Katika mchezo huo wa kirafiki uliochezwa Jumapili Desemba 27,2020 Timu ya Netiboli mkoa wa Manyara iliifunga mchezo timu ya Shule ya Sekondari Ayalagaya Magoli 42-15.
No comments:
Post a Comment