Watu 40 wameripotiwa kufariki baada ya mashua waliyokuwa wakisafiria kuzama mkoani Cabo Delgado nchini Mozambique.
Kulingana na taarifa za vyombo vya habari vya ndani, mashua hiyo iliyokuwa imebeba watu 74 kutoka pwani ya Palma ya Mozambique inayopakana na Tanzania, ilizama katika eneo la karibu na Kisiwa cha Ibo.
Watu 40 walipoteza maisha baada ya kuzama kwa mashua hiyo na wengine 32 waliweza kuokolewa.
Mashua hiyo inasemekana kusafirisha watu wengi waliokuwa wakitoroka kutokana na ongezeko la mashambulizi ya kigaidi upande wa kaskazini mwa nchi.
Jeshi la nchi limekuwa likiendesha operesheni kali za mara kwa mara tangu kutokea kwa mashambulizi ya makundi ya silaha miaka 3 iliyopita katika mkoa wa Cabo Delgado wenye idadi ya wakaazi milioni 2.3 na vyanzo vya gesi asili na madini mbalimbali.
Watu 400,000 wamelazimika kuhama makaazi yao kutokana na mashambulizi ya kigaidi na operesheni za kijeshi mkoani Cabo Delgado.
Ndani ya wiki jana pekee, watu 10,000 walikimbilia mji wa Pemba kwa kutumia usafiri wa mashua.

No comments:
Post a Comment