Kiongozi wa jimbo lenye mzozo la Tigray nchini Ethiopia Debretsion Gebremichael, amethibitisha leo kuwa wamefyetua makombora kuelekea mji mkuu wa taifa jirani la Eritrea na kuonya mashambulizi hayo huenda yataendelea.
Akizungumza kwenye mahojiano na shirika la habari la Associated Press, Gebremichael, hakusema ni makombora mangapi yamerushwa kwenye mji wa Asmara jana Jumamosi lakini amethibitisha kuwa mji huo ndiyo pekee uliolengwa nchini Eritrea.
Duru zimearifu makombora yasiyopungua matatu yalionekana kuulenga uwanja wa ndege kwenye mji huo mkuu, saa kadhaa tangu serikali hiyo ya mkoa wa Tigray ilipoonya juu ya uwezekano wa kufanya mashambulizi jana Jumamosi.
Mashambulizi hayo ni ishara pana ya kuzidi mvutano katika wakati mapambano yanaendelea kati ya vikosi vya jimbo la Tigray na serikali kuu mjini Addis Abbaba inayowashuhutumu viongozi wa eneo hilo kwa "uhaini"

No comments:
Post a Comment