Mwanasoka Diego Maradona amefanyiwa mazishi katika sherehe ya kibinafsi katika mji wa Buenos Aires nchini Argentina siku moja baada ya kufariki dunia.
Jamaa na marafiki wa karibu tu ndio waliohudhuria mazishi yake.
Lakini awali, kundi kubwa la watu lilijitokeza kutoa heshima zao za mwisho wengi wakiwa wanabubujikwa na machozi na kuonesha upendo
Maradona alifariki dunia kwasababu ya mshtuko wa moyo akiwa na umri wa miaka 60.
Kifo chake kimesababisha watu kumuombeleza kote duniani lakini hakuna walioomboleza kama raia wa nchi yake waliomchukulia kama shujaa wa taifa.
"Walinikata miguu" na misemo mingine ya kukumbukwa kutoka kwa nyota wa Argentina
Jeneza la Maradona lilifunikwa bendera ya taifa na fulana ya mpira nambari 10 nafasi aliyocheza uwanjani - pia fulana hiyo ilikuwa inaoneshwa kwa umma katika makao ya rais.
Kufikia mchana, foleni ya waliokuwa wamekuja kutoa heshima zao za mwisho ilifika umbali wa zaidi ya kilomita moja na polisi ikakabiliana na waombolezaji walipokuwa wanajaribu kufunga kwasababu ya muda.
Aidha, kulikuwa na taarifa za waombolezaji kurushiwa mabomu ya kutoa machozi na risasi za mpira.
Mmoja wa waombolezaji aliona ni kana kwamba polisi wametumia nguvu kupitia kiasi.
"Tumepanga foleni bila fujo yoyote na ghafla polisi wakaanza kurusha risasi za mpira," anasema, akinukuliwa na shirika la habari la Reuters. "Haifai, Mimi nataka tu kumuaga Diego kwa mara ya mwisho."
Baadhi ya mashabiki walipiga makofi wengine wakilia walipokuwa wakipita karibu na jeneza la Maradona
Na hatimaye mamlaka haikuwa na budi zaidi ya kufunga zoezi la kuruhusu raia kutoa heshima zao za mwisho ili kudumisha amani.
Gari iliyokuwa imebeba mwili wake ilielekea eneo la makaburi la Bella Vista viungani mwa mji ambapo alizikwa kando na wazazi wake.

No comments:
Post a Comment