Na Omary Mngindo, Bagamoyo
UONGOZI wa juu wa Chama Cha Waganga wa Tiba Asili na Tiba Mbadala na Wakunga wa Jadi (CHAWATIATA), umesema utawasilisha ombi kwa Rais Dkt. John Magufuli, wapatiwe nafasi mbili kati ya kumi za Wabunge wa kuteuliwa.
Hatua ya uwepo wa wawakilishi hao inalenga kuongeza ufanisi katika huduma, kwani watapigania kupatikana kwa kiwanda cha kutengeneza dawa, madaktari pamoja na maduka makubwa ya kuuzia dawa hizo.
Hayo yameelezwa Nov 18 na Mwenyekiti wa chama hicho Mkoa wa Pwani Salimu Mashimba, mbele ya wana-CHAWATIATA wa Bagamoyo baada ya kumalizika uchaguzi wa viongozi wake watakiongoza kwa miaka mitano ijayo.
"Uongozi wa juu wa Chama Cha Waganga wa Tiba Asili na Tiba Mbadala na Wakunga wa Jadi (CHAWATIATA), utawasilisha ombi kwa Rais Dkt. John Magufuli ili ikiwezekana tupatiwe nafasi mbili kati ya kumi za Wabunge wa kuteuliwa," alisema Mashimba.
Aidha wanachama hao wamepongeza Rais Dkt. John Magufuli kuchaguliwa kwa kishindo, pili hotuba nzuri alipohutubia Bunge, ambapo alisema anatambua huduma inayotolewa na waganga wa tiba mbadala.
Alisema kuwa Rais Magufuli amefanya mambo mengi makubwa, ikiwemo vita ya ugonjwa wa Corona ambapo Rais aliwataka wa-Tanzania kufanya ibada za kumuomba mungu, huku wakitumia dawa za miti, ambazo zimefanikisha kudhibiti ugonjwa huo.
"Pia aliwahimiza waumini wa dini kufanya ibada, kwa kushirikiana na wataalamu wa tiba mbadala na wengine mbalimbali hatimae Corona imebaki katika nchi nyingine, kwetu tumenusurika na ugonjwa huo," alisema Dkt. Mashimba.
Katika uchaguzi huo uliofanyika wilayani hapa chini ya Mashimba, Mratibu wa tiba asili Mganga Mkuu wa wilaya (DMO) akiwakilishwa na Dr. Ally Ponza, Rajabu Kisukali amechaguliwa tena kuwa Mwenyekiti wa chama hiyo wilaya ya Bagamoyo.
Makamu Mwenyekiti amechaguliwa Said Mbena, Katibu Mkuu Abuu Issa, Katibu Msaidizi Margareth Silas huku Katibu Mwenezi akienda kwa Said Juma wakati Mhazini amechaguliwa Salma Majani.
Upande wa Wajumbe ni wamechaguliwa Juma Magumila, Juma Doto, Gervas Kengere, Matata Said, Mrisho Fikiri na Haji Misungwi.
Akizungumza baada ya uchaguzi huo, Kisukali amewataka wanachama hao kuwabaini waganga wanaofika katika maeneo yao na kufanya shughuli zinazochafua taaluma yao kwani inawaondolea uaminifu kwa jamii.

No comments:
Post a Comment