Kampeni za Bobi Wine zilikatizwa Jumatano baada ya kukamatwa katika eneo la Luuka na kupelekwa kituo cha polisi cha Nalufenya.
Katika ujumbe aliouweka hii leo kwenye mtandao wa Twitter, Bobi Wine ameashiria kutokata tamaa ya kile anachotaka kufikia.
Kwa mujibu wa msemaji wa chama chake cha NUP Joel Ssenyonyi, Bobi Wine atarejelea kampeni zake Jumatatu 23, Novemba katika eneo la Kyenjojo na Fort portal.
Pia inasemekana kwamba kuna mipango ya kupanga tena kampeni katika maeneo alikotakiwa kufika kabla ya kukamatwa.
Baada ya kuchiwa huru, Bobi Wine alisema wafuasi wake wamejitolea kuendelea kupigania mabadiliko nchini humo na kuongeza kuwa hatua ya kuongezwa kwa maafisa wa usalama ni ishara ya uoga, hofu na ukosefu wa matumiani.
Bobi Wine alifanya maombi maalum na kutuma rambi rambi zake kwa familia zilizopoteza wapendwa wao wakati wa vurugu zilizotokea wiki jana baada ya kukamatwa kwake.
Jumamosi asubuhi, magari ya vikosi vya usalama yaliegeshwa katika maeneo tofauti mjini Kampala huku polisi wakishika doria katika maeneo karibu na makao makuu ya chama cha upinzani cha People's Power.
Polisi imetangaza kuwa ni watu 28 waliofarika katika maandamano ya siku ya Jumatano na Alhamisi, japo vyombo vya habari nchini Uganda vinanukuu vyanzo vya hospitali kuu kwamba idadi ya waliofariki ni watu 37.
Bobi Wine aliachiwa kwa dhamana siku ya Ijumaa, baada ya kushtakiwa kwa kukiuka kanuni za kudhibiti kusambaa kwa virusi vya corona.
Anakabiliwa na kifungo cha hadi miaka saba gerezani akipatikana na makosa.

No comments:
Post a Comment