Mabaa na maeneo mengine ya kuuza vileo yatafungwa na mikusanyiko ya kijamii itapunguzwa kwa kiasi kikubwa nchini Ujerumani chini ya msururu wa hatua kali mpya za kupambana na virusi vya corona wakati serikali ikijaribu kusitisha viwango vinavyoongozeka vya maambukizi.
Mipango hiyo itawasilishwa leo wakati Kansela Angela Merkel atakapofanya mkutano wa video na mawaziri wakuu wa majimbo 16 ya nchi.
Chini ya kanuni hizo mpya, ambazo huenda zikaanza kutekelezwa Novemba 4 hadi mwisho wa mwezi huo, watu wataruhusiwa tu kukutana katika maeneo ya umma na jamaa zao wanaoshi katika nyumba moja na kaya nyingine moja.
Mabaa, vilabu na maeneo ya aina hiyo yatafunguliwa tu kwa ajili ya huduma za kununua bidhaa za kufungiwa.
Shule na vituo vya malezi ya watoto vitaendelea kuhudumu lakini chini ya kanuni mpya za usafi. Tangu kuanza kwa janga la corona, kuna karibu visa 450,000 vya maambukizi nchini Ujerumani na zaidi ya vifo 10,000.

No comments:
Post a Comment