Search This Blog

Sunday, October 4, 2020

TAKUKURU yawaonya viongozi wa vyama vya msingi AMCOS

 



Na Hamisi Nasri, Masasi.   

WAKATI msimu wa korosho kwa mwaka 2020/2021 ukitarajia kuanza wiki ijayo Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na rushwa nchini (TAKUKURU) imewaonya vikali viongozi wa vyama vya msingi (AMCOS) mkoani Mtwara kuhakikisha wanatenda haki katika kusimamia vema malipo ya zao la korosho kwa wakulima wanaolima zao hilo ili waweze kulipwa kwa wakati.  

Aidha,Taasisi hiyo imesema  kuwa kiongozi yoyote ambaye atasababisha wakulima wa zao hilo la korosho kutolipwa fedha zao kwa madai ya kula kushwa sheria itachukua mkondo wake katika kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria kwa kutuhuma za rushwa.   

Onyo hilo limetolewa jana wilayani Masasi mkoani hapa na mkurugenzi mkuu wa TAKUKURU nchini,Brigedia Jenerali,John Mbungo wakati alipokuwa akizindua rasmi jengo jipya la Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na rushwa la wilaya ya Masasi mkoani hapa ikiwa ni utekelezaji wa agizo la rais Dkt.John Magufuli alilolitoa Julai 22,2020 jijini Dodoma kuwa majengo yote ya TAKUKURU mapya yazinduliwe.   

 Jenerali Mbungo alisema kuwa viongozi hao wa vyama vya msingi mkoani Mtwara ikiwemo wilaya ya Masasi lazima wawe makini katika utendaji kazi wao katika kusimamia malipo ya fedha ya korosho kwa wakulima wao ili kuepuka makosa yaliyofanyika kwa misimu ya korosho iliyopita ambapo baadhi ya wakulima hawakulipwa fedha zao.  

 Alisema Taasisi ya TAKUKURU nchini inatoa onyo kali kwa viongozi wa AMCOS wote wa mikoa ambayo inalima korosho kuwa iwapo watajihusisha na vitendo vya rushwa na kupelekea wakulima kushindwa kulipwa fedha zao kuwa wachukuliwa hatua za kisheria ili kulinda haki ya wakulima. 

Jenerali Mbungo alisema kuwa vitendo vya rushwa vinavyofanywa na baadhi ya viongozi wa vyama vya msingi kwenye vyama vyao vinasababisha haki ya wakulima kupotea ikiwemo kutolipwa malipo yao ya korosho kwa wakati hivyo kwa sasa katika msimu wa 2020/ 2021 TAKUKURU imejipanga kusimamia haki ya wakulima wa korosho.

 “Kuna jitahida kubwa zimeshafanyika katika kuokoa fedha za wakulima ambazo zilikuwa zimeibiwa na baadhi ya viongozi wa vyama vya msingi na tayari wakulima wamesharejeshewa fedha zao TAKUKURU bado inajipanga kuhakikisha fedha zote zilizobaki zinapatikana na wanarejeshewa wakulima,”alisema Jenerali Mbungo   

Akizungumzia kuhusu uzinduzi huo wa jengo jipya la ofisi ya TAKUKURU wilaya ya Masasi,Jenerali Mbungo alisema serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na rais Dkt. John Magufuli imefanya kazi kubwa ya kuimarisha na kuendeleza mapambano dhidi ya rushwa na ufisadi hapa nchini. 

Jenerali Mbungo alisema upatikanaji wa jengo hilo jipya la wilaya ya Masasi na mengine ambayo yamejengwa katika wilaya zingine nchini ambapo jumla ya majengo hayo yapo saba nchini ni wazi kuwa yataongeza ufanisi wa utendaji kazi dhidi ya vitendo vya rushwa.  

Akizungumza katika uzinduzi huo wa jengo jipya la TAKUKURU wilaya ya Masasi kwa niaba ya mkuu wa mkoa wa Mtwara,Gelasius Byakanwa, mkuu wa wilaya ya Masasi, Selemani Mzee alisema  aliwataka wananchi wa mkoa wa Mtwara kutoa ushirikiano wa karibu kwa Taasisi hiyo kuzuia na kupambana na rushwa katika kudhibti vitendo vya rushwa.



No comments:

Post a Comment

Punguza kilo tano kwa siku saba

  NI watu wachache wanaopenda kunenepa, wengi wanapenda miili ya wastani kwa kuwa  unene si mzuri. Ukiwa mnene si tu kwamba unakaribisha m...