Waziri wa mambo ya kigeni wa Ufaransa Jean-Yves Le Drian aliye ziarani nchini Mali, leo ameondoa uwezekano wa kufanyika mazungumzo na makundi ya itakadi kali yanayoendesha uasi kwenye taifa hilo la kanda ya Sahel.
Mwanadiplomasia huyo amesema msimamo wake wa kukataa mazungumzo na waasi, unaungwa mkono na Baraza la Usalama la Umoja wa mataifa na kundi la mataifa matano ya kanda ya Saleh yaliunganisha nguvu kupambana na ugaidi.
Ziara ya Le Drian ambayo ni ya kwanza kufanywa na afisa wa ngazi ya juu wa serikali ya Ufaransa tangu kutokea mapinduzi ya kijeshi nchini Mali mwezi Agosti inakuja katika wakati viongozi wa ulimwengu wanatafakari uwezekano wa kufanya mazungumzo na makundi ya waasi.
Mapigano makali yanaendelea nchini Mali licha ya kuweko kwa vikosi vya jeshi la Ufaransa na Umoja wa Mataifa, hali iliyochochea miito ya kutaka kufanyika mazungumzo na makundi ya wapiganaji ili kumaliza umwagaji wa damu.

No comments:
Post a Comment