Na Ahmad Mmow, Lindi.
Mgombea ubunge wa jimbo la Lindi kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Amida Abdallah amesema serikali imedhamiria kutekeleza ujenzi wa mtambo wa kuchakata gesi asilia ( LNG) mtaa wa Likong'o, manispaa ya Lindi. Kwahiyo wanaosema haina mpango wa kutekeleza mradi huo ni waongo.
Amida alitoa kauli hiyo jana katika mtaa wa Kariakoo, kata ya Rasbura, manispaa ya Lindi wakati wa mkutano wa kampeni za uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika tarehe 28.10.2020.
Mgombea huyo ambae ni kati ya wagombea ubunge wawili wanawake miongoni mwa majimbo nane yaliyopo mkoani Lindi alisema siyo kweli kwamba serikali haina nia ya kutekeleza mradi huo kama ambavyo baadhi ya wagombea wanafasi hiyo na viongozi wa vyama vyao wanavyotangaza kwenye mikutano yao ya kampeni. Bali serikali imedhamiria kutekeleza mradi huo mkubwa ambao unatarajia kutoa ajira za moja kwa moja na mbadala kwa wananchi wa wilaya ya Lindi na nyingine za Mkoa wa Lindi.
Alisema ushahidi unaothibitisha kama serikali imedhamiria kwa dhati kutekeleza mradi huo nikufanya malipo ya fidia kwa wananchi walioachia maeneo yao ili kupisha ujenzi wa mtambo huo katika mitaa ya Likong'o na Mtomkavu. Ulipaji ambao yeye alisimamia kutokanana kuwa mjumbe wa kamati ya nishati ya bunge la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania.
Alisema kutokana na ukweli huo, wagombea wanaosema wakichaguliwa kuwa wà bunge wataisukuma serikali itekeleze wanawadanganya wananchi. Kwani serikali haiitaji kusukumwa katika jambo ambalo yenyewe kwa hiyari yake imeanza kutekeleza.
Alibainisha kwamba ahadi ya serikali kwa wananchi wa mikoa ya Lindi na Mtwara kunufaika na ugunduzi wa gesi asilia iliyogunduliwa katika mikoa hiyo inatekelezwa. Ushahidi wa hilo ni serikali kuzindua mpango wa matumizi ya gesi asilia majumbani. Mpango ambao ulizinduliwa hivi karibuni na waziri mwenye dhamana ya nishati( Dkt Merdard Kalemani) katika mtaa wa Mnazimoja, manispaa ya Lindi.
Mbali na hayo, mgombea huyo alisema iwapo wananchi watampa ridhaa yakuwa mbunge wao atasimamia utapatikanaji ajira na maendeleo endelevu katika jimbo hilo kwakutumia fursa zinazotokanana maliasili na rasilimali zilizopo katika jimbo hilo.
Aidha alisema iwapo atachaguliwa na kuwa mbunge atahakikisha linajengwa soko la kisasa na kuongeza barabara za mitaa za kiwango cha lami zenye urefu wa kilometa kumi baada tu yakuanza kuwatumikia wananchi kwa nafasi hiyo ya ubunge.
" Lakini pia nitasimamia na kuhakikisha kinajengwa kituo cha kisasa cha mabasi ambacho nitakuwa na uwezo wa kuingiza mabasi miatano. Kituo hicho kitajengwa katika kata hii ya Rsbura, lakini vilevile nitahakikisha ujenzi wa zahanati ile unakamilika. Nikitangazwa tu nimeshinda nitaanza kuchangia mifuko miamoja ya saruji," Amida aliahidi.
Ujenzi wa mtambo wa kuchakata gesi asilia umekuwa kama miongoni mwa kete muhimu kwa wagombea wa ubunge wa jimbo la Lindi. Kwani wagombea wote wanautaja na kuuzungumzia mradi huo kama ni miongoni mwa miradi itakayotoa ajira zitakazosababisha fursa za mtambo huo. Hata hivyo kila mgombea anauzungumzia kwa mtazamo wake.

No comments:
Post a Comment