Akizungumza katika hafla ya kukabidhiana madawati huko katika Skuli ya Dkt Salmin Amour Juma, Chumbuni Mjini Unguja amesema ni fursa ya kila raia kupata haki yake ya Msingi ya Elimu ambapo Serikali imekuwa ikihakikisha inapatikana bure kuanzia Maandalizi, Msingi na Sekondari ya lazima katika mazingira mazuri.
Mhe Haroun ambae pia ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Utumishi wa Umma na Utawala bora amesema Elimu bure lazima iende sambamba na mazingira mazuri kwa watumishi wote hivyo amesema ana imani kuwa Walimu wataongeza bidii ya ufundishaji kutokana na kuwepo mazingira mazuri ya ufundishaji.
Aidha amewaomba wananchi kuunga mkono juhudi kubwa za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar zinazofanywa katika nyanja mbalimbali hasa za kielimu kwa kuwahamasisha Vijana wao kusoma ili malengo ya Serikali ya kuwa na wataalamu wake hapa nchini yaweze kufikiwa.
Pia Mhe Haroun ameutaka uongozi wa Wizara ya Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa, Idara Maalum na Vikosi vya SMZ, kuhakikisha wanayawekea alama maalum madawati yote na kuhakikisha hayatumiki kinyume na malengo yaliyokusudiwa ili yasipotee na yadumu kwa muda mrefu na kuwasaidia watoto wao.
Kwa upande wake Makamo Mwenyewekiti wa Kamati hiyo na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Mhe Riziki Pembe Juma amesema mashirikiano mazuri baina ya kamati ya madawati na Wizara ya Elimu ni miongoni mwa njia za mafanikio ya kupunguza tatizo la madawati nchini.
Aidha Mhe Riziki amewataka viongozi wa halmashauri kushirikiana na Walimu wa Skuli za Msingi ili kuhakikisha madawati hayo yanagawiwa kwa wakati ili wanafunzi ambao hawana vikalio waweze kufaidika na vikalio hivyo
Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu Utawala na Uendeshaji Bwana Abdullah Mzee Abdullah amesema ni agizo la Mhe Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi DK Ali Mohamed Shein la kutafuta madawati ili kuhakikisha tatizo hilo linapungua na kila Mwanafunzi anasoma katika mazingira mazuri na ya kuridhisha.
Jumla ya makontena 9 yenye madawati 4495 kwa ajili ya Wanafunzi wa madarasa ya Msingi
ya mekabidhiwa ikiwa ni ya awamu ya tatu.

No comments:
Post a Comment