Search This Blog

Sunday, August 16, 2020

Nyuki kudhibiti Tembo mashamba ya Bagamoyo Sugar

Na Omary Mngindo, Makurunge


MIZINGA ya nyuki inataraji kuwekwa katika mpaka wa mashamba ya Miwa ya Kampuni ya Bagamoyo Sugar, hususani upande unaopakana na Hifadhi ya Mbuga ya Saadani, ikiwa ni mikakati ya kudhibiti Tembo.


Shamba hilo linalomilikiwa na Kampuni ya Bakhresa Group chini ya Mkurugenzi Said Bakhresa, lina ukubwa wa ekta elfu kumi ambapo malengo yake ni uzalishaji wa sukari, ambapo kwa sasa ujenzi wa majengo mbalimbali ukiendelea, huku kazi kubwa ikiwa imeshafanuika.


Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi Mahusiano Makampuni hayo Hussein Sufiani, akitoa taarifa mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhandisi Evarist Ndikilo akiwa eneo la mradi Agost 15, huku uongozi wa juu wa Kampuni hiyo ukiongozwa na Abubakar Bakhresa.


Kauli ya Sufiani imetanguliwa na swali lililoulizwa na Mhandisi Ndikilo, aliyeanza kwa kusema kuwa akiwa Mkuu wa wilaya katika moja ya wilaya mkoani Morogoro kulikuwa na changamoto kubwa ya tembo kuingia kwenye mashamba ya miwa, huku akitaka kujua mikakati ya Kampuni.


Baada ya swali hilo Sufiani alisema kwamba katika kujihami huko wanataraji kuweka mizinga ya nyuki katika mpaka unaopakana na Hifadhi ya Taifa ya Saadani, ambako ndiko wanakopatikana wanyama hao wakali, wanaopenda sana kula miwa.


"Katika kujihami na matukio ya Tembo kuingia ndani ya mashamba yetu kula miwa tumejipanga kikamilifu, tunataraji kuandaa mizinga ya nyuki itayowekwa katika miti kando ya mashamba yetu na Hifadhi ya Taifa ya Saadani, nadhani hiyo itakuwa hatua nzuri ya kuwadhibiti wanyama hao hatari" alisema Sufiani.


Alisema kuwa ujenzi wa mradi huo unaojengwa kwa awamu tofauti, tayari wa-Tanzania 600 wananufaika na mradi, ambapo alieleza kuwa uzalishaji utakapoanza kwa msimu wanataraji kuzalisha tani 35,000, huku akieleza kuwa wanataraji kusaidia ongezeko la uchumi kwa wana-Bagamoyo, Mkoa na nchi kwa ujumla.


Ndikilo akiambatana na Katibu Tawala Dkt. Delifine Magere na Kamati ya Ulinzi na Usalama, alipokelewa na Zainab Kawawa, Katibu Tawala Kasilda Mgeni na Kamati ya Ulinzi na usalama ya Wilaya, ambapo alimpongeza Rais John Magufuli kwa kuwaletea Mradi huo mkubwa.


Alisema kuwa Rais Magufuli aliamua kuupatia uongozi wa Kampuni hiyo eneo hilo kwa lengo la kuendelezwa kwa kilimo cha miwa, juhudi ambazo zimeshaanza kuleta matunda kwa wana-Bagamoyo, Mkoa na nchi kwa ujumla kutokana na kuwepo kwa wa-Tanzania 600 waliotangulia kupata ridhiki kupitia mradi huo.


"Matunda ya Rais Magufuli kuipatia ardhi hii Kampuni ya Bakhresa Group yanaanza kuonekanna, kwani mbali ya kuwepo kwa ajira ya kutosha pia uzalishaji huu utaotengeneza upatikanaaji wa bidhaa hiyo hapa nchini, nitumie nafasi hii mumshukuru sana Rais," alisema Mhandisi Ndikilo.


Kwa upande wake Kawawa aliupongeza uongozi huo kwa mafunzo waliyowapatia Madiwani waliomaliza muda, ambao waliwapeleka kujifunza kwenye viwanda vinavayozalisha miwa na kutengeneza sukari mkoani Morogoro ambayo wamepatiwa wana-Bagamoyo.




No comments:

Post a Comment

Punguza kilo tano kwa siku saba

  NI watu wachache wanaopenda kunenepa, wengi wanapenda miili ya wastani kwa kuwa  unene si mzuri. Ukiwa mnene si tu kwamba unakaribisha m...