Maelfu ya waandamanaji walimiminika katika barabara karibu na makazi rasmi ya waziri mkuu wa Israeli Benjamin Netanyahu katika eneo la Kati la Jerusalem jana usiku wakionesha tena upinzani wao wakati maandamano ya wiki kadhaa dhidi ya kiongozi huyo yakikosa kuonyesha dalili ya kupungua.
Katika kipindi chote cha msimu wa kiangazi, maelfu ya raia wa Israeli wamekuwa wakifanya maandamano ya kumtaka Netanyahu ajiuzulu huku wakilalamika kuhusu jinsi anavyolishughulikia janga la virusi vya corona na kusema hapaswi kuwa ofisini wakati anapokabiliwa na kesi ya mashtaka ya ufisadi.
Wafanyabiashara ambao biashara zao ziliathirika kutokana na janga la virusi vya corona pia walishiriki katika maandamano ya jana.Ijapokuwa Netanyahu amejaribu kupuuza maandamano hayo, yaonekana kuongezeka nguvu.
Maandamano hayo dhidi ya Netanyahu ni makubwa zaidi kushuhudiwa nchini Israeli tangu maandamano ya mwaka 2011 yaliochochewa na kuongezeka kwa gharama ya maisha.

No comments:
Post a Comment