Search This Blog

Wednesday, August 19, 2020

Kesi za uchaguzi kumaliza ndani ya miezi minne

 Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi

amewataka Majaji wa Mahakama Kuu kuwa tayari kusikiliza mashauri

yatakayofunguliwa kutokana na uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika mwezi

Oktoba mwaka huu.

Akifunga awamu ya kwanza ya mafunzo ya namna bora ya uendeshaji wa

mashauri ya uchaguzi kwa baadhi ya waheshimiwa Majaji wa Mahakama Kuu ya

Tanzania, Jaji Kiongozi amesema Mahakama itampangia Jaji yeyote kusikiliza

mashauri ya uchaguzi hivyo kila Jaji anapaswa kuwa na hali ya utayari na

kujiandaa kutekeleza wajibu huo muhimu.

“Mafunzo mliyopata yana lengo la kuweka mazingira sahihi ili Jaji yeyote

atakapopangiwa kusikiliza mashauri yatokanayo na uchaguzi Mkuu awe tayari

wakati wote”, alisisitiza Jaji Kiongozi.

Alisema Mahakama imepanga kumaliza mashauri yatakayotokana na uchaguzi

Mkuu wa mwaka huu ndani ya miezi minne (4) kwa kuwa tayari imeshaonesha

mwelekeo wa kuyashughulikia. Aliongeza kuwa katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka

2015 mashauri ya aiona hiyo yalisikilizwa na kumalizika ndani ya miezi sita (6)

tangu kufunguliwa kwake.

Jaji Feleshi amewataka Majaji Wafawidhi kujiandaa na pia kuhakikisha

wanawaandaa Naibu Wasajili pamoja na Mahakimu ili wawe tayari kusikiliza

mashauri hayo. Kiongozi huyo pia ameagiza mashauri mengine yaliyopo na

yanayoendelea kufunguliwa mahakamani yaendelee kusikilizwa na kumalizika

kwa wakati licha ya kuwepo kwa mashauri yatakayotokana na uchaguzi Mkuu.

Aidha, ametoa wito kwa Majaji wote kuendeleza ushirikiano uliopo baina yao,

kujaliana na kupendana wakati wote kwa kuwa mahakama ni familia.

Mafunzo hayo yaliyoandaliwa na Mahakama ya Tanzania kwa kushirikiana na

Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) yamesaidia kuwajengea uwezo

Maafisa wa Mahakama na kuwaandaa kutoa haki kwenye mashauri ya Uchaguzi

Mkuu ujao wa Rais, Wabunge na Madiwani.

Mafunzo yaliyomalizika leo yaliwahusisha baadhi ya Waheshimiwa Majaji wa

Mahakama Kuu ya Tanzania. Awamu inayofuata pia itawahusisha Majaji wengine


wa Mahakama Kuu ya Tanzania na Jumatatu Agosti 24 yataanza mafunzo hayo

kwa Wasajili, Naibu Wasajili na Mahakimu Wakazi Wafawidhi wa Mahakama za

Hakimu Mkazi.

Mafunzo haya pia yatatolewa kwa waheshimiwa Majaji wa Mahakama ya Rufani

kuanzia Septemba 2-4, 2020 mkoani Morogoro. Mahakimu Wakazi Wafawidhi wa

Mahakama za Wilaya nao watapatiwa mafunzo hayo baadaye katika Chuo cha

Uongozi wa Mahakama Lushoto-Tanga.

Wawezeshaji wa mafunzo hayo ni baadhi ya Majaji wa Mahakama ya Rufani na

Mahakama Kuu waliopo na wastaafu, Naibu wasajili, Mahakimu pamoja na

wawezeshaji kutoka Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Taasisi ya Kuzuia na

Kupambana na Rushwa, Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa na Tume ya

Kurekebisha Sheria ambao ni wadau muhumu katika masuala ya Uchaguzi.



No comments:

Post a Comment

Punguza kilo tano kwa siku saba

  NI watu wachache wanaopenda kunenepa, wengi wanapenda miili ya wastani kwa kuwa  unene si mzuri. Ukiwa mnene si tu kwamba unakaribisha m...