
MBAO FC,mambo yashakuwa magumu kwa upande wao kwenye Ligi Kuu na benchi la ufundi na wachezaji wa kikosi hicho wamekiri wazi kuwa wanahitaji kukomaa ili wapate ushindi katika mechi nane zilizobaki kwa sasa ili wajinusuru na janga la kushuka daraja.
Juzi jumapili Mbao ilikubali kichapo cha mabao 2-0 ambacho kimeifanya isalie na pointi zake 22 wakishika nafasi ya 19 katika msimamo wa Ligi Kuu.
Wakizungumza na Mwanaspoti Online,wachezaji wa kikosi hicho na Benchi la ufundi walisema ni wakati sasa wa kupambana kuweza kuinusuru timu hiyo kubaki ligi kuu msimu ujao.
“Tuko katika nafasi mbaya sana haswa baada ya kichapo na Azam lakini niseme bado tuna nafasi kubwa tusahau ule mchezo sasa tujikite kwenye hii michezo Nane iliyobakia ya ligi.
Kikubwa tunatakiwa tusikate tamaa tuendelee kukomaa na ule mchezo na Azam usije kutuvuruga tukubali tushapoteza na sasa tujipange kwa Coastal Union,”alisema Straika Ndaki Robert.
Winga wa timu hiyo Herbert Lukindo alisema sasa kinachotakiwa ni wao wachezaji kujitoa sana ili kuweza kuinusuru timu hiyo kubaki ligi kuu msimu ujao.
“Tunachotakiwa ni kutokata tamaa maana bado tuna nafasi kubwa ya kubaki ligi kuu msimu iwapo tutashinda mechi Sita za nyumbani kisha mbili za ugenini tukitafuta angalau sare,” alisema Lukindo.
Kocha Msaidizi wa timu hiyo,Agustino Malindi alisema akili zao sasa zipo katika mchezo wao na Coastal Union ambapo utapigwa Juni 23 katika uwanja wa CCM Kirumba kuhakikisha wanapata pointi tatu.
“Tuko Mwanza tayari kikubwa tunachokifanya ni kuangalia mapungufu kwenye kikosi chetu haswa eneo la ulinzi na ushambuliaji na kuweza kurekebisha kasoro hizo ili tuwe tayari kwa mchezo wetu na Coastal Union,” alisema Malindi.
Mbao wamebakiza mechi nane ambapo sita zitakuwa nyumbani dhidi ya timu za Coastal Union,Polisi Tanzania,Lipuli,Mtibwa Sugar,Namungo na Ndanda huku mbili watacheza ugenini dhidi ya JKT Tanzania na Simba.
No comments:
Post a Comment