Search This Blog

Sunday, June 21, 2020

Kufutwa jina la Marekani katika azimio la kupinga ubaguzi wa rangi la Umoja wa Mataifa



Wakati maandamano ya kupinga ubaguzi wa rangi uliokita mizizi nchini Marekani yakiendelea kurindima kote duniani na hasira zilizosababishwa na mauaji ya kikatili yaliyofanywa na polisi mzungu dhidi ya Mmarekani mweusi zikiwa bado kali, maafisa wa serikali ya Washington wanafanya jitihada kubwa za kuzima harakati ya kimataifa ya kupinga ubaguzi.

Katika mkondo huo huo jina la Marekani limefutwa katika azimio la kupinga ubaguzi wa rangi la Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa.

Baada ya mabadiliko hayo, Baraza la Haki za Binadamu la UN limelaani ubaguzi wa rangi wa kimfumo na ukatili unaofanywa na polisi bila hata ya kuashiria jina la Marekani. Muswada wa azimio hilo ambao ulikuwa na jina la Marekani kama kituo kikuu cha ubaguzi wa rangi na ukatili wa polisi duniani, ulitayarishwa na kuwasilishwa na nchi za Afrika zikiungwa mkono na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Muswada huo ulitoa wito wa kufanyika uchunguzi kuhusu ubaguzi wa rangi unaofanyika kimfumo na kwa mpangilio maalumu huko Marekani na katika nchi nyingine.


Jina la Marekani limefutwa katika azimio la Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa huku nchi hiyo ikiendelea kushuhudia maandamano makubwa ya kupinga ubaguzi wa rangi dhidi ya raia wenye asili ya Afrika kwa karibu wiki nne mfululizo. Maandamano hayo yalianza baada ya polisi mzungu kumuua kikatili Mmarekani mweusi, George Floyd hapo tarehe 25 Mei katika mji wa Minneapolis jimboni Minnesota.

 Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa, Michelle Bachelet ameyataja mauaji yaliyofanywa na polisi mzungu wa Marekani dhidi ya George Floyd kuwa ni "ukatili uliokita mizizi" na nembo ya ubaguzi wa kimfumo na kuongeza kuwa: "Ukatili huu wa sasa unatokana na ubaguzi wa rangi wa kimfumo na siasa za kibaguzi na zilizofeli za kukabiliana na turathi ya kipindi cha biashara ya utumwa na ukoloni."


Kufutwa jina la Marekani katika azimio la Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa kumewakasirisha wanaharakati wengi wa kupambana na ubaguzi wa rangi kwa sababu historia ya nchi hiyo ni ushahidi tosha wa ubaguzi wa rangi ambao umekuwa ukifanyika nchini humo katika vipindi vyote ambao umefikia kileleni katika utawala wa rais wa sasa wa nchi hiyo, Donald Trump. Kiongozi huyo amekuwa akimahasisha na kuunga mkono waziwazi ubaguzi wa rangi na katika hotuba zake nyngi amekuwa akikariri waziwazi na kwa njia isiyo ya moja kwa moja kwamba, wazungu ndio kizazi cha juu na bora zaidi! Trump alikwenda mbali zaidi na kuwataja watu wanaoandamana kupinga mauaji ya kikatili ya George Floyd kuwa ni wahuni na watu wanaopenda ghasia na ametoa wito wa kukabiliana nao.

Prf. Gerald Horne ambaye ni mwandishi, mwanahistoria na mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Houston ameashiria historia chafu ya ukatili wa polisi na askari usalama wa Marekani dhidi ya wasio wazungu na kusema: "Mzizi na chanzo cha ukatili huu ni kipindi cha biashara ya utumwa. Waafrika hawakuja Marekani kwa irada na matakwa yao wenyewe bali waliburutwa na kuletwa America na wazungu kama watumwa. Haya ni maafa makubwa sana tunayoishi ndani yake.”


Azimio la kupinga ubaguzi wa rangi limepasishwa baada ya kufanyika mabadiliko makubwa katika muswada wake wa awali licha ya jitihada kubwa zilizofanyika ili vipengee vyake muhimu vipasishwe likiwemo jina la Marekani kama kituo kikuu cha ubaguzi wa rangi duniani. Suala hilo limezikasirisha sana taasisi na jumuiya za kutetea haki za binadamu ambazo zimekosoa harakati kubwa zilizofanywa na Marekani iliyotumia ushawishi wake kwa ajili ya kuondolewa vipengee hivyo.

Jamil Dakwar ambaye ni Mkurugenzi wa Mpango wa Haki za Binadamu wa Jumuiya ya Haki za Kiraia ya Marekani (HRP) anasema: “Marekani imeunga mkono tena ukatili wa polisi dhidi ya watu weusi kwa kutumia mabavu dhidi ya nchi nyingine kwa shabaha ya kufuta jina la nchi hii katika azimio la kupinga ubaguzi wa rangi na kudhoofisha azimio hilo la kihistoria.”

Ukweli ni kwamba, ubaguzi wa rangi nchini Marekani ni hakika chungu ambayo si rahisi kuikanusha au kuificha kwa kutumia ushawishi na mabavu, na ubaguzi huo umekuwa sulubu kwa jamii za waliowachache na wasio wazungu hususan Wamarekani wenye asili ya Afrika. Kwa msingi huo kufutwa jina la Marekani katika azimio la Baraza la Haki za Bindamu la Umoja wa Mataifa la kupinga ubaguzi pia hakuwezi kuficha ukweli wa mambo kuhusu maradhi hayo sugu yanayondelea kuisumbua jamii ya nchi hiyo. 



No comments:

Post a Comment

Punguza kilo tano kwa siku saba

  NI watu wachache wanaopenda kunenepa, wengi wanapenda miili ya wastani kwa kuwa  unene si mzuri. Ukiwa mnene si tu kwamba unakaribisha m...