
SIMBA na Yanga zimeafikiana na wazo la kurejesha Ligi Kuu Bara chini ya uangalizi na utaratibu maalumu na wote wamesisitiza kwamba ngoma sasa iwekwe uwanjani mbivu na mbichi zijulikane.
Ligi Kuu Bara ambayo ilisimama mwezi Machi inatazamiwa kuanza wiki ya kwanza ya mwezi Juni, kulingana na mapendekezo yaliyowasishwa serikalini.
Viongozi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na wale wa Bodi ya Ligi (TPLB) walikutana juzi Jumapili jioni, katika kikao kilichotumia saa mbili ili kujadili namna ligi itakavyoendelea pale itakapopewa baraka na Rais John Magufuli.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi, Almas Kasongo aliliambia Mwanaspoti: “Tulipendekeza ifanyike ikiwa na watu wachache, katika mapendekezo yetu tumeipeleka iwe wiki ya katikati ya Juni, lakini itategemea na maelekezo ya Serikali.
”Hivyo kama mapendekezo hayo yakipita inamaanisha kwamba kuanzia wiki hii klabu zitakuwa na wiki nne na ushee za kupiga matizi na kujipanga upya ndani na nje ya uwanja. “Tumependekeza pia mashabiki hawataruhusiwa kwenda uwanjani na badala yake wataangalia kwenye runinga wakiwa majumbani kwao,” alisema huku akisisitiza kutakuwa na idadi ndogo ya viongozi na waandishi wa habari ambao watapimwa na kukaa umbali stahiki kwa mujibu wa kanuni za afya. “Kikao kimetengeneza azimio la kwanza ni ligi zote kurejea pale ambapo tuliishia na tutacheza katika mfumo uleule ambao tulikuwa tunacheza hapo awali kwa maana ya timu kuwa nyumbani na ugenini,” alisema.
Kasongo alisema walikuwa na azimio la pili kuunga mkono na kwenda katika utekekezaji mara
moja agizo la Rais kuona utaratibu gani unatumika ili ligi zote kuweza kurejea mara moja.
“Nafikiri ndani ya siku mbili tatu tutakuwa tumeshakamilisha na kuwapatia wenzetu Wizara ya
Michezo mapendekezo yetu kabla ya kushea na Rais JPM kwa ajili ya utekelezaji na kuendelea pale ambapo tuliishia.”
SIMBA NA YANGA
Kocha wa Yanga, Luc Eymael aliposikia kwamba msimu wa kimashindano kwa maana Ligi Kuu Bara na mashindano mengine unaweza ukarudi, amefurahia sana na kusisitiza hicho ndicho alichokuwa akisubiri kusikia.
Awali Luc kabla ya tamko la Serikali aliwahi kupendekeza kupitia Mwanaspoti kwamba wachezaji kadhaa wa kila timu wapimwe na kuweka karantini na kuendelea na mashindano mbalimbali na wasiruhusiwe kwenda popote. “Kwangu niwapongeze wote wenye mamlaka ya hili kwani kwa mtazamo wangu wamefanya uamuzi sahihi ambao nina imani wametenga muda wa kutosha mpaka kufikia katika uamuzi huo,” alisema Eymael ambaye anaendelea na mchakato wa kuisuka Yanga mpya ya msimu ujao huku wadhamini GSM wakisisitiza hawatanunua mchezaji yeyote wa kukaa benchi.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa Simba, Senzo Mazingisa alisema ni jambo zuri kwa wenye mamlaka kufikia hatua ya kurudisha ligi na wao wanasubiri kauli kamili kutoka kwao.
“Ni jambo ambalo tulikuwa tukilisubiri kwa muda mrefu ingawa bado halijatimia ila tumeona mwanga kwamba muda wowote ligi itarudi kwa kufuata utaratibu ambao tutapatiwa,” alisema Senzo.
Ofisa Habari wa Simba, Haji Manara, kwenye mitandao ya kijamii amezisifu mamlaka kwa uamuzi makini huku akiwasisitiza Yanga: “Sasa tukutane uwanjani, tujue mjanja nani..hakuna kubebana hapa.”
No comments:
Post a Comment