Search This Blog

Monday, May 25, 2020

Naibu waziri Kanyasu akerwa na Wavamizi Mapito ya wanyamapori


Na John Walter-Manyara

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Constantine Kanyasu amekerwa na wananchi wanaojenga nyumba na kuendesha shughuli za kilimo katika maeneo yenye wanyamapori hasa katika mapito ya wanyamapori katika eneo la Kwakunchinja linalounganisha Hifadhi ya Taifa ya Tarangire na Hifadhi ya Manyara.

Amesema kutokana na tabia hiyo, serikali haiwezi kumaliza kulipa vifuta jasho na vifuta machozi kwa wananchi wanaoshambuliwa na wanyamapori wakali na waharibifu.

Akizungumza na viongozi wa Jumuiya ya Hifadhi ya Wanyamapori ya Burunge (WMA) Wilaya ya Babati  mkoani Manyara, amesema ni vyema sasa Viongozi hao kutafakari na  kuona namna ya kulinda ushoroba wa eneo la  Kwakunchinja ambao ni muhimu kwa wanyamapori wanaotoka Hifadhi ya Taifa ya Tarangire kuelekea Hifadhi ya Ziwa Manyara.

Ameeleza kuwa, mwaka 2020  pekee, serikali imetumia Shilingi bilioni moja katika kulipa vifuta jasho na vifuta machozi  kwa wananchi huku Sh bilioni 2.3 zikiwa hazijalipwa kwa wananchi walioathiriwa na wanyamapori wakali na waharibifu.

Kanyasu amesema kila mahali wananchi wamekuwa wakilalamika kuchelewa kulipwa vifuta jasho na vifuta machozi kutokana na madai hayo kuwa mengi hali inayosababisha wizara kuwa na madai mengi yasiyolipika kutoka kwa wananchi ambao baadhi wameyafuata makazi ya wanyamapori.


Amesema serikali inatafuta mbinu mbadala ya kupunguza migogoro baina ya binadamu na wanyamapori wakali na waharibifu baada ya kugundua fidia sio suluhisho kutokana na wimbi kubwa la wananchi kuendesha shughuli za kibinadamu shoroba za wanyamapori na maeneo ya mitawanyiko ya wanyamapori.

Amesema kutokana na baadhi ya wananchi kufanya makazi maeneo hayo, wizara imegundua hata ikitenga bajeti nzima ya wizara kwa ajili ya kulipa vifuta jasho na vifuta machozi haitaweza kumaliza tatizo hilo.

Alisema binadamu wamekuwa wakiwafuata wanyamapori hivyo suala la mazao ya kushambuliwa ni jambo lisiloepukika.

 “Sehemu ya Mapori ya Akiba na Jumuiya ya Hifadhi za Wanyamapori ndimo wananchi wameanzisha makazi hivi unategemea wanyamapori watulie tu,” alihoji Kanyasu.
Aidha ameshauri kuwekwa Kamera,mabango yanayohimiza madaerava kuendesha mwendo wa taratibu na kuanisha faini zinazopasa kutozwa kwa atakaeua Mnyama wakati akiendesha maeneo ya hifadhi.

Amemtaka Mkuu wa wilaya ya Babati, Elizabeth Kitundu kuhakikisha anawatumia watendaji wa vijiji vilivyoko jirani na hifadhi kuhakikisha wanazuia uuzaji maeneo ya mapitio ya wanyamapori kwa wananchi.

Mkuu wa wilaya ya Babati Elizabeth Kitundu, akifunga kikao hicho muhimu alimuahidi Naibu waziri kuwa amepokea maagizo hayo na kinachofuata ni utekelezaji ili kuhakikisha rasilimali hiyo muhimu ya Wanyamapori inaendelea kuwepo katika hifadhi hizo.

No comments:

Post a Comment

Punguza kilo tano kwa siku saba

  NI watu wachache wanaopenda kunenepa, wengi wanapenda miili ya wastani kwa kuwa  unene si mzuri. Ukiwa mnene si tu kwamba unakaribisha m...