
Dar es Salaam. Mashabiki wa Klabu ya Yanga wanaweza kuwa na sababu ya kuanza kutabasamu kufuatia taarifa za uongozi wa timu hiyo kwa kushirikiana na mdhamini wao, GSM, kuwa katika hatua za mwisho za usajili wa beki wa kati wa Coastal Union, Bakari Mwamnyeto.
Taarifa kutoka ndani ya Coastal Union zinasema uongozi wao utakutana na ule wa Yanga pamoja na GSM mwishoni mwa wiki hii ili kukamilisha ‘dili’ hilo ili mwakani Mwamnyeto ambaye pia ni beki wa timu ya Taifa ‘Taifa Stars’, aanze kuitumikia timu hiyo.
Awali, mchezaji huyo alikuwa pia akiwaniwa na watani zao, Simba. Hata hivyo, baada ya kupigana vikumbo tokea dirisha dogo la usajili la Januari, Simba inaonekana kuachana na mbio za kumsajili na kuangalia wachezaji wengine.
Taarifa zinasema mazungumzo hayo yalikuwa yamshirikishe meneja wa mchezaji huyo, Kassa Mussa, ambaye hata hivyo hataweza kuhudhuria kutokana na kukwama nchini Italia kutokana na kutokuwepo usafiri wa ndege wa moja kwa moja kwa sababu ya ugonjwa wa corona.
Kassa ni mtu muhimu katika ‘dili’ hilo, lakini Italia imezuia safari za ndege kuingia na kutoka kama ilivyo Tanzania.
“Mpaka sasa naweza kusema kuwa Mwamnyeto amefikia hatua nzuri sana kuichezea Yanga msimu ujao, mazungumzo yameenda vizuri na baadhi ya timu kubwa ambazo zilikuwa zinamtaka zimeshindwa kuendelea na mazungumzo,” kilisema chanzo cha Mwananchi.
“Kiukweli, Mwamnyeto mbali ya kuwa na meneja ni mali ya Coastal Union, hata hivyo mchango wa Kassa Mussa ambaye ndiye meneja wake unatambulika na pande zote tatu Yanga, Coastal Union na mchezaji mwenyewe.”
Chanzo hicho kilisema hakuna meneja au wakala mwingine anayetambulika na klabu na mchezaji mwenyewe zaidi ya Kassa ambaye enzi zake aliwahi kuichezea Coastal Union.
Mwamnyeto mwenyewe alikiri kuwa Yanga imefikia hatua za mwisho ili ajiunge nayo.
Alisema kuwa kama mchezaji hana pingamizi endapo taratibu zote zitafuatwa na yeye kupata stahiki zake kwa mujibu wa matakwa yake. “Mpira ni kazi yangu, nina malengo ambayo nimejiwekea, naweza kucheza nchi na klabu yoyote ambayo itatimiza matakwa kwa mujibu wa utaratibu ambao tumejiwekea mimi, klabu na meneja wangu,” alisema.
Kwa upande wake, makamu mwenyekiti wa Coastal Union, Hassan Muhsin alisema mazungumzo kati yao na Yanga yamefikia pazuri na wana matumaini kuwa Mwamnyeto atajiunga na klabu hiyo kongwe.
“Ni kweli kuwa kuna kikao wikiendi hii Dar es Salaam kuhusiana na suala hilo, mimi sitakuwepo, ila viongozi wengine watakuwepo na kujadiliana masuala mbalimbali,” alisema.
No comments:
Post a Comment