
London, England. Klabu za Ligi Kuu England (EPL) zinafikiria kuendelea na msimu huu wa ligi mwezi ujao ili kuepuka kupata hasara ya Pauni 750 milioni kutoka kwenye haki ya matangazo ya televisheni.
Keshokutwa wawakilishi wa klabu zote 20 za EPL watafanya mkutano kwa njia ya video na washika dau pamoja na bosi wa EPL, Richard Masters ili kupata njia bora zaidi ya kuendelea na msimu.
Kwa mujibu wa mtandao wa Daily Mail, klabu zitasukuma msimu uendelee tena Mei, ambapo mechi zitachezwa bila ya mashabiki ili kufikia mwisho Julai 16. Jambo hilo litazifanya kuokoa fedha walizopata kutokana na haki ya matangazo ya kumalizia msimu.
Televisheni za Sky na BT zimenunua haki ya matangazo kwa Pauni 3 bilioni ambazo zitafika mwisho Julai 31, huku msimu mwingine ukitarajiwa kuanza siku inayofuata.
Iwapo kutakuwa na kikwazo televisheni hizo zinaweza kugoma kulipa fedha zilizobaki msimu huu kama timu hazitacheza ndani ya muda na sasa klabu zinatazama uwezekano wa kurudi kuendelea na msimu.
Bosi mmoja wa Ligi Kuu England alikaririwa na Daily Mail akisema: “Kama hatutmaliza msimu huu tutatakiwa kurudisha Pauni 750 milioni kwenye kampuni za televisheni.
“Kama hatutacheza msimu ujao tutapoteza Pauni 3 bilioni.Hili limekuwa suala muhimu na hapo tunapaswa kuchangua njia iliyo salama. Na kama hatutaanza msimu hadi Oktoba, tutakuwa kwenye wakati mgumu wa kumaliza msimu mzima na kwenda na muda wa kuanza kwa michuano ya Ulaya mwakani.”
No comments:
Post a Comment