Search This Blog

Wednesday, April 22, 2020

JABIR: Lile bao langu kwa Brazil si mchezo

By OLIVER ALBERT

Ni Jabir Aziz Stima. Ukimuona ana mwili fulani mdogo, lakini ni fundi kwelikweli uwanjani. Na ana rekodi ambayo miaka nenda rudi haiwezi kufutika.

Ndiye kiungo pekee Afrika Mashariki na Kati mwenye rekodi ya pekee ambayo hakuna mchezaji aliyeiweka zaidi yake katika ukanda huu ya kuifunga timu bora ya Taifa duniani (enzi hizo), Brazil kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Juni 7, 2010. Licha ya timu ya Taifa ‘Taifa Stars’ kupokea kichapo cha mabao 5-1, lakini hakikuzuia furaha ya Watanzania kufurahia bao maridadi la kichwa alilofunga Jabir dakika ya 87.

Mabao ya Brazil yalifungwa na Robinho dakika ya 10 na 34, Ramires dakika za 53 na 92 na Ricardo Kaka dakika ya 76. Jabir hakuanza  katika kikosi cha kwanza, lakini aliingia dakika ya 78 akichukua nafasi ya Abdulharim Humud na kisha kwenda kuandika rekodi hiyo.

Bao la Jabir lilikuwa la kwanza ambalo ngome ya Brazil iliruhusu katika mechi kumi ilizocheza wakati ikijiandaa kwa fainali za Kombe la Dunia  zilizofanyika Afrika Kusini. 

Jabir anasema bao hilo limebaki kama alama na kumbukumbu kwake na hata katika mioyo ya Watanzania.

“Nilijisikia vizuri sana nilipofunga lile bao kwani ukizingatia tulicheza na timu bora duniani, hivyo kufunga mbele ya wachezaji nyota ni jambo ambalo sitalisahau.

Advertisement

“Ni bao ambalo liliniongezea thamani kwa watu kwani mpaka leo bado wanalikumbuka na pia liliniongezea thamani hata kwa klabu yangu niliyokuwa naichezea wakati huo Azam FC,” anasema Jabir ambaye awali aling’ara na Simba.

Hata hivyo, Jabir anakiri kuwa kupata nafasi tu katika mchezo huo ni jambo ambalo hatalisahau kutokana na ushindani wa namba uliokuwepo katika kikosi cha Stars hasa nafasi ya kiungo anayocheza.

“Kila mchezaji katika kile kikosi alikuwa na hamu ya kucheza dhidi ya Brazil. Nilikuwa napambana   mazoezini ili kumshawishi kocha wa wakati huo, Marcio Maximo,  anipange na nashukuru licha ya kwamba sikuanza lakini niliingia na kufunga bao,” anasema Jabir ambaye ni miongoni mwa wachezaji wanaoibeba JKT Tanzania kwa sasa. 

“Wakati naingia Kocha Maximo aliniambia kuwa jiamini, nenda kacheze mpira uonekane kwani unawakabili wachezaji wakubwa duniani, hivyo kuwa makini na upambane sana, na nilitekeleza alichoniambia kwa sababu mpira ulipomalizika alifurahi sana.”

AMKUBALI RAMIRES

Jabir anasema licha ya kuvutiwa na wachezaji wote wa Brazil waliocheza mchezo huo, lakini alivutiwa zaidi na Ramires kutokana na alivyokuwa akicheza na kupambana uwanjani.

Anasema licha ya kupitia mikononi mwa makocha wengi lakini Maximo  alikuwa kocha wa kipekee kwake.

“Ni kocha wa kipekee sana kwani ndiye aliyesababisha Watanzania wanifahamu nikiwa bado na umri mdogo na mpaka leo wananizungumza kwa sababu yake.

“Nakumbuka alikuwa akinikubali sana tangu nacheza Ashanti United na alipanga kuniita  timu ya Taifa, lakini akaja kugundua kuwa nimecheza mechi chache, hivyo bado nahitaji kupata uzoefu akaniambia niendelee kucheza kwani ananifuatilia.

“Nilipotoka Ashanti na kujiunga na Simba tu akaniita tena timu ya Taifa kwani tayari nilishapata uzoefu.Hivyo ni kocha ambaye sitamsahau kwani alikubali uwezo wangu tena nikiwa nachezea timu ndogo,” anasema Jabir.

KWA MABINTI SASA

Humwambii kitu kwa mabinti hawa. Jabir anasema licha ya kuwepo na viungo wengi wazuri  kwenye Ligi Kuu Bara lakini anavutiwa zaidi na viungo wa timu ya wanawake ya JKT Queen,  Fatuma Issa ‘Bekham’ na Etoo Mlenzi. “Huwa navutiwa sana na jinsi wanawake hawa wanavyoitendea haki nafasi ya kiungo hasa huyo Fatuma ni fundi sana.”

NJE YA BONGO

Jabir anasema hakuna jambo analolifurahi hivi sasa kama kuona wachezaji wengi wa Tanzania wakitoka kwenda kucheza soka la kulipwa nje ya nchi. “Nafurahi kuona wachezaji wengi wanatoka sasa hivi tofauti na zamani. Naamini wanavyocheza huko wakirejea wanakuja na kitu kipya cha kujifunza na wanakuwa msaada kwa timu ya Taifa,” anasema.

Jabir anasema hajapata nafasi hiyo ya kwenda kucheza soka nje ya nchi, lakini  kama ikitokea kwa sasa yupo tayari kwenda.

JAMBO LILILOMUUMIZA

 Desemba 26, 2009  Simba ilikuwa iikabili Tusker ya Kenya katika mchezo wa kuwania mshindi wa tatu wa kkombe la Tusker, Jabir alionekana akitoka  uwanjani  huku ameinamisha kichwa akilia kiasi cha  baadhi ya wachezaji wenzake kumpiga piga mgongoni wakimtuliza wakati akielekea nje ya uwanja kubadilisha na Nico Nyagawa aliyeingia kuchukua nafasi yake dakika ya 29 ya mchezo huo.

Si kwamba alikuwa akilia kwa maumivu ya nyonga aliyopata siku hiyo , lakini  ile hali ya kucheza dakika chache za mchezo huo. “Kwanza kabla ya ule mchezo nilikuwa nje ya uwanja muda mrefu kutokana na kusumbuliwa na matatizo ya misuli ya tumbo, hivyo ndio nilikuwa nimerejea uwanjani na nakumbuka nilicheza baadhi ha mechi za kawaida na mechi ngumu ya kwanza kwangu ilikuwa hiyo dhidi ya Tusker,” anasema Jabir ambaye anaamini Mungu akijalia janga la corona limalizike JKT Tanzania itarejea uwanjani ikiwa kwenye ubora wake na watamaliza msimu vizuri kama walivyoanza.

“Lakini ghafla nikajikuta nacheza muda mfupi baada ya kupata maumivu ya nyonga na kutolewa. Yaani ile siku niliumia sana maana najiona niko fiti halafu nashangaa napata tena maumivu. Niliumia sana ndio maana hadi machozi yalinitoka.”

Jabir amemuoa Jasmeen na wana watoto watatu, wakiwamo pacha Nizar na Nadir pamoja na Najma.

“Hao mapacha niliwapa majina hayo kwa sababu ya kuwapa heshima kaka zangu niliokuwa nawakubali sana kwenye soka Nadir Haroub ‘Canavaro’ na Nizar Khalfan.”

Jabir alianza soka la ushindani 2008  akiichezea Ashanti United iliyomsajili kutoka timu ya Friends Rangers.

Mwaka 2008 alijiunga na Simba aliyoichezea kwa misimu miwili kabla ya mwaka 2010 kusajiliwa na Azam FC aliyoitumikia hadi mwaka 2014 kisha akaenda JKT Tanzania, Mwadui, Ndanda na sasa anaichezwa JKT Tanzania.

Let's block ads! (Why?)

No comments:

Post a Comment

Punguza kilo tano kwa siku saba

  NI watu wachache wanaopenda kunenepa, wengi wanapenda miili ya wastani kwa kuwa  unene si mzuri. Ukiwa mnene si tu kwamba unakaribisha m...