
KOCHA wa Yanga, Luc Eymael amesema kwamba anapofanya usajili au kutoa maelekezo mchezaji fulani asajiliwe huwa habahatishi.
Amesema hata mchezaji kiraka Mnyarwanda, Ally Niyonzima wa Rayon Sports hakupendekeza asajiliwe kutokana na uswahiba wake na Haruna Niyonzima, bali ni fundi na anayebisha basi asubiri kuona makali yake kwenye Uwanja wa Taifa msimu ujao iwapo kweli Yanga itafanikiwa kufikia dau na kumchukua.
“Nimempitisha Niyonzima kutokana na kutaka mchezaji ambaye anaweza kucheza katika eneo la kiungo wa kukaba na kushambulia ambapo mchezaji huyo anaweza na muda mwingine kucheza kama mlinzi wa kati, ni sifa ya ziada hiyo kwa maana hiyo kwangu amepita na nimebariki usajili wake kama atapatikana,” alisema kocha huyo ambaye ana majina zaidi ya kumi mapya kwenye faili lake na asilimia kubwa ameshaanza nao mazungumzo ya awali.
“Ana uwezo wa kucheza na viungo waliopo sasa Haruna Niyonzima, Papy Kabamba Tshishimbi na wengineo ambao hata kama ikitokea mmojawao amekosekana pia kwa kupewa kadi, adhabu au hata kuumwa anaweza kwenda kuziba nafasi hiyo na mambo yakawa mazuri.
“Kwa maana hiyo tukifanikiwa kumpata Niyonzima atakuja kuongeza kitu ndani ya Yanga na kuimarisha eneo la kiungo kuwa bora zaidi ya msimu huu.
“Kutokana na mapendekezo yangu nimetaka mchezaji mwenye uwezo wa aina yake kusajiliwa ili kuja kuimarisha eneo hilo, labda tatizo inaweza kuwa kwenye gharama na ishu za mikataba, lakini ngoja tuone,” alisema Eymael ambaye ameagiza wachezaji asilimia kubwa wa kikosi cha kwanza waongezewe mikataba haraka.
“Kuhusu ubora wake na tofauti yake Niyonzima hilo nadhani ni baada ya kumpata,” alisema Eymael ambaye aliongeza kuwa huko Ubelgiji kwao baadhi ya maduka ya vyakula yamefunguliwa na wananchi wachache wachache wameruhusiwa kutembea kwa vibali maalumu kutokana na ishu ya corona.
Kocha wa zamani wa Simba, Mrundi Masoud Djuma alisema mchezaji huyo aliwahi kumfundisha katika klabu ya AS Kigali 2017-18 na alikuwa akimtumia katika kikosi cha kwanza kwenye nafasi tatu tofauti uwanjani kutokana na umahiri ambao alikuwa akiuonyesha kwenye timu na kama Yanga wakimpata itakuwa freshi kwao.
Ally hana uhusiano wa damu wa moja kwa moja na Haruna Niyonzima, lakini ni ndugu kiukoo, na wanafahamiana. Kwa upande wake, Haruna amesema jamaa anajua kuuchezea mpira kama akiweza kuhimili presha za mashabiki Jangwani.
No comments:
Post a Comment