
LONDON, ENGLAND . MIKEL Arteta na Ole Gunnar Solskjaer kila mmoja anatafuta njia ya kuwatuliza mashabiki wake.
Wanafahamu hakuna namna nzuri kwa sasa ya kutuliza mashabiki zaidi ya kufanya usajili wa nguvu hasa kwa kipindi hiki ambacho suala la kubeba ubingwa imekuwa shida. Shughuli ni pevu kote, Arsenal na Manchester United.
Kocha Arteta amesema kwamba mpango wake ni kuongeza walau wachezaji watatu kwenye kikosi chake, lakini ametia shaka makubwa kama atakabidhiwa pesa ya kufanya hivyo kwenye dirisha lijalo. Kocha huyo Mhispaniola alisema hafahamu kama mabosi wake watampa pesa ya kusajili au watamwaacha tu aendelee kutumia wachezaji waliopo kwenye sasa kwenye kikoisi chake.
Arteta alisema: “Nimepanga kufanya usajili wa wachezaji wawili au watatu hivi, lakini tunakabiliwa na mambo mengi ambayo yanatufanya tuwe kwenye mashaka makubwa kama tutasajili au la. Hatufahamu. Hatufahamu hali ya kipesa tulipo kwa sasa, hatujui dirisha litafunguliwa lini. Tuna vitu vingi ambavyo vipo nje ya uwezo wetu kwa sasa."
Kwa upande wa mpinzani wake huko Man United, kocha Solskjaer ameripotiwa kwamba atakabidhiwa mkwanja wa Pauni 150 milioni kufanya usajili kwenye dirisha lijalo. Lakini, mpango wake ni kunasa mastaa wasiopungua watatu, ambao wote thamani yao inazidi hiyo Pauni 150 milioni. Sambamba na hilo, janga la corona limesababisha mtikisiko mkubwa wa kiuchumi na kumfanya kwamba kama anahitaji nyota hao, basi ni lazima apige bei mataa wasiopungua watano, wakiapo Paul Pogba, Alexis Sanchez, Jesse Lingard, Phil Jones na Chris Smalling ili kupata pesa ya kusajili mastaa anaowataka.
Arteta anahitaji kuimarisha timu yake kwenye beki na ndio maana wachezaji anaohusishwa nao ni Samuel Umtiti, Corentin Tolisso na Jesse Lingard, wakati Solskjaer naye, anasaka wachezaji wa maeneo hayo, ambapo kwa siku za karibuni amekuwa akihusishwa na Jadon Sancho, Kalidou Koulibaly na Saul Niguez.
Kwenye Ligi Kuu England, kama ligi haitarudi na kuendelea msimu huu, Man United itapoteza Pauni 48 milioni kwenye mapato ya televisheni, Pauni 17.6 milioni kwenye viingilio na Pauni 50.8 milioni kwenye dili za kibiashara na kuwafanya kuwa na hasara ya Pauni 116.4 milioni kutokana na jambo hilo, wakati Arsenal wao wanapoteza Pauni 40 milioni kwenye dili za televisheni, Pauni 15.4 milioni kwenye viiingilio na Pauni 19.4 milioni kwenye dili za kibiashahara na kuwafanya wawe na hasara ya Pauni 74.8 milioni. Jambo hilo linafanya dili za makocha wa timu hizo mbili kuwa kwenye mashaka makubwa ya kukamilika hasa kutokana na janga hilo la maambukizi ya corona.
No comments:
Post a Comment