Search This Blog

Saturday, March 21, 2020

Walipo wapinzani wa Kagere mbio za ufungaji msimu uliopita

Dar es Salaam. Wakati Meddie Kagere akizidi kutesa katika ufungaji wa mabao kwa msimu wa pili kwenye Ligi Kuu Bara, washambuliaji wenzake waliokuwa wakimfukuzia msimu uliopita ni kama wamepotea.
www.mwanaspoti.co.tz hili limebaini kuwa washambuliaji wengi waliong’ara katika ufungaji msimu uliopita  wameyumba msimu huu, huku baadhi yao majeraha yakiwa chanzo na wengine wakishindwa kuwashawishi makocha kutokana na viwango vyao.
Kagere ndiye aliyeibuka mfungaji bora msimu uliopita akifunga mabao 23, akifuatiwa na Salim Aiyee aliyekuwa Mwadui FC ambaye alifunga 18 wakati Heritier Makambo aliyekuwa Yanga alifunga 17 na John Bocco (Simba) alifunga mabao 16.
Wengine waliofuata ni aliyekuwa mshambuliaji wa Simba, Emmanuel Okwi (15), Dickson Ambundo wa Alliance (12) na Donald Ngoma wa Azam (11). Hata hivyo katika orodha hiyo ukiwaondoa Okwi, Makambo na Ambundo waliotimkia nchi nyingine,  Kagere ndiye aliyeendeleza moto msimu huu kwani mpaka sasa ametupia wavuni mabao 19.
Aiyee anayeichezea KMC msimu huu ambaye baadhi ya mashabiki walitarajia angeendelea kutisha msimu huu mambo yamekuwa tofauti kwani hadi ligi iliposimama wiki iliyopita alikuwa amefunga bao moja  alilofunga katika mchezo dhidi ya Yanga uliofanyika Machi 12.
Mchezaji huyo aliuanza msimu na majeraha, lakini hata alipopona alishindwa kupata nafasi kikosi cha kwanza cha KMC.
Hata hivyo, amesema sababu ya kuyumba ni majeraha na kwamba, bado hajakata tamaa.
“Sitakata tamaa licha ya kwamba sitaingia katika orodha ya wale ambao wana mabao mengi, lakini  angalau natamani nifanye kitu cha tofauti.,” alisema Aiyee.
“Sisi washambuliaji alama inayotufanya tutambulike ni kufunga mabao, sasa unaposhindwa kufanya hivyo inaumiza sana.”
Naye Bocco mpaka sasa ana mabao manne, lakini kama ilivyo kwa Aiyee anaweza kuwa na sababu baada ya kuwa nje kutokana na maumivu ya goti. Hata hivyo, baada ya matibabu ya muda mrefu na kurejea kikosini, nahodha huyo wa Simba amezinduka wakati ligi ikielekea mwishoni, hivyo ana kazi kubwa ya kuvunja rekodi yake ya msimu uliopita.
Kasi  ya Kagere imeonekana kuwa kubwa na kuwashinda washambuliaji wengi zaidi mwingine aliyefunikwa ni Ngoma ambaye ametangaza kuwa hataongeza mkataba na Azam msimu ujao akilenga kwenda kutafuta changamoto sehemu nyingine.
Ngoma amekuwa na wakati mgumu katika kikosi hicho kwa kuwa mwanzoni alikuwa akipewa nafasi ya kuanza, lakini ukame wa mabao uliwafanya makocha kumrejesha benchi. Mshambuliaji huyo wa zamani wa Yanga amefunga mabao  mawili  mpaka sasa, hivyo kuonekana kuwa yuko katika kiwango cha chini zaidi msimu huu ukilinganisha na msimu uliopita alipomaliza ligi akiwa na mabao 11.
Hawa wamo
Achana na Kagere, lakini kuna washambuliaji waliotamba msimu uliopita na sasa bado wamo.
Mshambuliaji wa Namungo FC, Bigirimana Blaise ambaye hadi sasa ana mabao tisa anadaiwa bao moja ili kuivunja rekodi  aliyojiwekea msimu uliopita alipomaliza akiwa na mabao 10 wakati akizichezea Stand United na Alliance FC.
Blaise amekuwa katika kiwango bora msimu huu akishirikiana na Reliants Lusajo mwenye mabao 11 na Lucas Kikoti aliyefunga manne.
Mwingine  ambaye  ameendeleza kasi ni Ayoub Lyanga wa Coastal Union aliyemaliza msimu uliopita na mabao 10 na hadi sasa anayo manane.
Akizungumzia ubora wa wachezaji hao, Kocha Kennedy Mwaisabula alisema Kagere ni mpambanaji akiwa pia na sifa ya kujiweka katika eneo zuri la ufungaji tofauti na wachezaji wazawa.

Let's block ads! (Why?)

No comments:

Post a Comment

Punguza kilo tano kwa siku saba

  NI watu wachache wanaopenda kunenepa, wengi wanapenda miili ya wastani kwa kuwa  unene si mzuri. Ukiwa mnene si tu kwamba unakaribisha m...