Search This Blog

Tuesday, March 24, 2020

Tegete gari linawaka,gari linazima

By Charity James

MWAKA 2006 hautakaa usahaulike kwa Jerryson John Tegete. Ni mwaka ambao aliichezea timu ya Taifa, Taifa Stars kwa mara ya kwanza, chini ya Kocha Mkuu Mbrazil Marcio Maximo.

Kwa nini hatausahau? Ni wazi kuitwa kwake huko, wengi walibeza kutokana na kutokuwa na jina na waliamini hataweza.

Hata hivyo, Kocha Maximo alipenda kumwita mara kwa mara Stars na kipindi hicho alikuwa akiichezea timu ya Makongo High School alikokuwa pia akisoma na kiwango chake kilikuwa bora zaidi.

Ni kama aliiva kwa Maximo kwani hata baada ya kuwa anaachwa nje ya Stars baada ya kocha huyo kutimka nchini, mwaka 2014 baada ya kurudi na kujiunga na mabingwa wa Kihistoria, Yanga, katika usajili wake alimwita tena na kujiunga na Wanajangwani hao.

Mwanaspoti lilifanya nmahojiano na nyota huyu wa Alliance FC na kuelezea maisha yake ya soka.

kACHEZA NDONDO KWA SH3 MILIONI

Advertisement

Usajili wa Ligi Daraja la Kwanza si zaidi ya Sh3 milioni. Hata hivyo, Tegete anafichua hiyo milioni tatu aliipata kwenye mechi moja tu ya mchangani baada ya bosi mmoja wa timu ya Mwanza United kuhitaji achezee kikosi chake.

“Nakumbuka bado nilikuwa Makongo, na kipindi cha likizo nilienda Mwanza nyumbani. Kuna bosi alikuwa anaisimamia timu ya Mwanza United aliniomba niichezee timu yake hiyo na kuniuliza nahitaji kiasi gani. Sikua najua sana hela na hivyo nikaropoka tu Sh3 milioni na aliiweka kwenye akaunti yangu ya benki niliyofunguliwa na mzee wangu kwa ajili ya matumizi ya shule na ada.”

NGASSA, CR7 WAMPA MCHONGO

Tegete anafichua mbali na kupenda soka tangu utotoni, lakini kuna nyota wawili waliochangia kumshawishi na kutaka kufuata nyayo zao. “Kwa upande wa wachezaji wa nje navutiwa na Ronaldo, ni mchezaji ambaye alinifanya nicheze nafasi ya ushambuliaji. Nilikuwa namtazama sana na mara nyingi nilikuwa naenda kurudia kile alichofanya kwenye mazoezi yangu. Naamini kuna mengi niliyafanikisha ndio maana bado nipo hapa nilipo.”

“Kwa upande wa wachezaji wa ndani basi mimi huniambii kitu kwa mshambuliaji Mrisho Ngassa. Ni mchezaji ninayempenda sana na nimekuwa nikimfuatilia. Pia alinipa changamoto ya kupambana zaidi hasa nilipocheza naye pamoja kipindi hicho nikiwa Yanga.”

STARS, YANGA ZIMEMBEBA

Kwenye maisha kutengeneza historia ni ngumu kama huna unachofanya, kujituma kwa Tegete kumemwingiza katika historia. Kwanza kuichezea Stars na pili kuvaa uzi wa Yanga. Anakiri ni kati ya mambo yatakayobaki kwenye kumbukumbu zake milele.

“Taifa Stars na Yanga zimeingia kwenye historia ya maisha yangu. kuitwa mara ya kwanza Stars sitakaa nisahau kwani mimi sijapita njia ndefu sana kama wengine maana kipaji changu kimeonekana nikiwa shule.”

“Kila mchezaji ana malengo ya siku moja kuichezea timu yake ya Taifa, pia kwa wachezaji wa ndani kila mmoja anatamani kucheza Simba na Yanga zikiwa ni njia nzuri za kupata mafanikio nje ya nchi japo sio wote wanapitia huko,” anasema na kuongeza, kwa Yanga hana ujanja kwani ndio timu iliyomtengenezea jina na ataiheshimu sana kumkuza kisoka.

YONDANI vs NYONI

“Erasto Nyoni ni kiraka ukiamka ukitaka acheze popote anacheza kwa sababu ana akili nyingi ya mpira, japo beki ya kati ndio anafanya vizuri zaidi, hata hivyo, tofauti na Kelvin Yondani kwangu Yondani ni zaidi kwenye nafasi hiyo.”

KUSTAAFU HAPANA

“Nilianza kucheza soka na kupata mafanikio nikiwa na umri mdogo, hivyo, kwa sasa bado sijafikiria kuacha soka kwani bado nina uwezo na nina mapenzi nalo na familia yangu inapenda pia soka.”

SOKA LATIBUA UANASHERIA

“Nimekuwa katika familia ya soka baba yangu alikuwa mwanasoka na sasa ni kocha alikuwa anapenda sana nicheze soka, hivyo kuingia huko vilikuwa ni vishawishi vya baba ambaye alimzidi nguvu mama ambaye alikuwa anatamani kuona mwanae nasoma,” anasema.

“Nilikuwa napenda sana kuwa mwanasheria lakini ndoto ilipotea baada ya kujikuta njia yangu nyeupe kufanikiwa kupitia soka,” anasema na kuongeza, tangu aanze soka hajawahi kula umeme (kadi nyekundu) kutokana na kuheshimu sheria 17 za soka.

MAXIMO BABA LAO

“Maximo alikuwa kocha mzuri sana, aliitengeneza Taifa Stars iliyoamsha hisia za kila Mtanzania na timu iliungwa mkono na kila mtu nchini. Alifanya kazi kubwa kuhakikisha timu inapendwa na kila mtu,” anasema Tegete.

“Licha ya kutokufanya vizuri kwenye Chan, kufuzu michuano ile ilikuwa mafanikio makubwa kwani yaliongeza umaarufu wetu nje ya mipaka ya Afrika,” anasema Tegete na kumalizia kwenye maisha yake hajawahi kujuta kuingia kwenye soka kwani amepata mafanikio makubwa kwenye soka ambayo hawezi kuweka wazi kwani hajafikia malengo aliyojiwekea.

Pia amewashauri wachezaji chipukizi na kuwahakikishia kuwa soka ni moja ya kazi yenye manufaa kwa wanaotambua na kuthamini wanachokifanya wawapo uwanjani huku akisisitiza haina mahitaji ya elimu ya darasani lakini mafanikio ni makubwa wakijituma.

Let's block ads! (Why?)

No comments:

Post a Comment

Punguza kilo tano kwa siku saba

  NI watu wachache wanaopenda kunenepa, wengi wanapenda miili ya wastani kwa kuwa  unene si mzuri. Ukiwa mnene si tu kwamba unakaribisha m...