SERIKALI mkoani Lindi, imekiri kudaiwa na wakulima Sh. 6,930,549,278 zikiwa ni malipo ya mauzo ya korosho, msimu uliopita 2018/2019 na kuwa ucheleweshaji huo umechangiwa na uhakiki.
Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Mkoa huo, Godfrey Zambi, wakati wa kikao cha Kamati ya Ushauri (RCC) kilichofanyika mjini hapa.
Zambi alisema hayo kufuatia wajumbe kutaka wapewe maelezo kinachokwamisha wakulima wa korosho mkoani humo kutolipwa fedha zinazotokana na uuzaji korosho kwa msimu wa mwaka 2018/2019.
Akijibu hoja za wajumbe hao, alisema katika madai hayo, wapo wakulima waliokwisha lipwa sehemu ya fedha zao na wengine bado hawajalipwa huku akitaja sababu kubwa kuwa ni utaratibu wa uhakiki.
Aliwaambia wajumbe wa kikao hicho kwamba wakulima wa korosho ambao bado hawajalipwa wanadai Sh. 4,869,550,801 huku waliopunguziwa kulipwa wanadai Sh. 1,224,493,477.
Akitaja viwango kwa kila halmashauri, alisema Liwale ndiyo inayoongoza wakulima wake kudai Sh. 1,771,544,094 ikifuatia Nachingwea, Sh. 1,605,348,226, Ruangwa Sh. 1,398,682,428, Lindi Vijijini Sh. 669, 973,916, Kilwa Sh. 599,544,924 wakati Manispaa ya Lindi, wakidai Sh. 48,453,690.
Alisema ucheleweshwaji huo, umechangiwa na mambo mbalimbali, yakiwamo uhakiki ili kuwafahamu wahusika halisi wanaostahili kulipwa fedha hizo, huku akisisitiza serikali kutambua deni la wakulima hao na litalipwa fedha zitakapopatikana.
“Tunajua wamechelewa kulipwa, lakini tunawaomba wavumilie na pale fedha itakapopatikana watalipwa,” Zambi alisisitiza.
Awali, wakichangia hoja katika kikao hicho, wabunge Hamidu Bobari (Mchinga), Mohamedi Kuchauka (Liwale) na Selemani Said Bungara (Bwege) (Kilwa kusini), walihoji sababu za wakulima wa korosho kuchelewa kulipwa fedha zao zinazotokana na uuzaji wa zao hilo, msimu wa mwaka 2018/2019.

No comments:
Post a Comment