
Mwanza. Mbao inayoshiriki Ligi Kuu Tanzania Bara imewekwa sokoni kwa Sh350 milioni.
Kauli hiyo imetolewa na mwenyekiti wa klabu hiyo Solly Njashi jana alipokuwa akizungumzia mustakabali wa Mbao katika ushiriki wake wa ligi hiyo.
Mbao inayopambana na janga la kutoshuka daraja msimu ujao, ipo nafasi ya 19 ikiwa na pointi 23 kwenye msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Njashi alisema jukumu la kwanza ni kuinusuru Mbao kushuka daraja msimu ujao na endapo hali itakuwa mbaya wataiweka sokoni kwa Sh350 milioni.
Mwenyekiti huyo alisema hawana fedha za kutoa huduma kwa timu hiyo kutokana na mtikisiko wa kiuchumi ulioikumba klabu hiyo.
“Lazima tuwe na uamuzi mgumu tunaendelea kusaka wadau ili kutupa nguvu timu ibaki Ligi Kuu kama tutakosa, tutaiuza kwa sababu tatizo kubwa ni fedha,” alisema Njashi.
Wakati mwenyekiti huyo akitangaza kuiweka sokoni klabu hiyo, baadhi ya wadau akiwemo Juma Hussein alisema ni vyema uwepo utaratibu wa mgawanyo wa fedha za mauzo.
“Tunajua mpira ni fedha viongozi wamepambana, lakini uwepo utaratibu ambao kila upande atanufaika, sisi wadau tunapenda timu ibaki hapa Mwanza hata ikiuzwa,” alisema Hussein.
Fulgence Dickson alisema ni vyema uongozi ukaitisha mkutano wa dharura kujadili mustakabali wa klabu hiyo kabla ya kuiweka sokoni.
No comments:
Post a Comment